Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa sana leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KIPI MUHIMU ZAIDI KWAKO…
Kila mtu anataka muda zaidi,
Kila mtu ana mambo mengi ya kufanya kuliko muda uliopo,
Kila mtu anapoteza muda!
Na hii ni kwa sababu watu wamekuwa wanayapa uzito sawa mambo yote wanayotaka kufanya.
Wanafanya bila ya kutafakari uzito na umuhimu wa mambo, hivyo yale mambo ya kawaida na yasiyo muhimu, yanachukua nafasi ya mambo mazito na ya muhimu.
Sawa na kukaa kuangalia taarifa ya habari kwenye TV wakati hujasoma kitabu. Au kuperuzi mitandao ya kijamii wakati hujakamilisha majukumu yako makubwa ya siku.
Katika kuhakikisha unatumia muda wako vizuri, muda huo mdogo ulionao ambao kila kitu kinaugombania, fanya yafuatayo;
Kwanza jiulize ni maeneo gani kwenye maisha yako unataka kupiga hatua kubwa.
Kisha orodhesha mambo yote unayopaswa kufanya na yale unayopenda kufanya hata kama hayana mchango kwenye mafanikio yako.
Baada ya hapo weka muda ulionao katika kufanya mambo yako.
Halafu sasa anza kugawa muda wako kwa yale mambo ambayo ni muhimu zaidi, ambayo yatakufikisha kwenye mafanikio unayotaka.
Hayo ndiyo mambo muhimu na ndiyo yanastahili muda wako.
Mengine hata yakikosa muda hakuna tatizo, kama unafanya yale muhimu, hayo mengine yatajipanga yenyewe.
Usikubali mambo yasiyo muhimu yashike nafasi ya yale mambo muhimu kwako. Panga kufanya mambo yako kulingana na umuhimu wake, na utaweza kuutumia muda wako vizuri.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.