Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Ni siku nyingine nzuri na ya kipekee ambapo tumepata nafasi ya kipekee ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USHINDI UNALETA USHINDI ZAIDI…
Kila kitu tunachofanya kwenye maisha yetu kinaambukiza, matokeo unayopata yanachochea na kushawishi matokeo zaidi.
Kile unachoangalia kwenye maisha, na kukifikiri kwa muda mrefu ndiyo kinakua zaidi kwenye maisha yako.
Na ndiyo maana wale tunaoona wamefanikiwa wanazidi kufanikiwa,
Matajiri wanazidi kuwa matajiri,
Na masikini wanaendelea kuwa masikini.
Kile unachopata kinavutia kuendelea kupata hicho zaidi na zaidi.
Kama kwa sasa unapata ushindi, utaendelea kuvutia ushindi zaidi na zaidi.
Lakini kama sasa unapata matokeo mabaya, kama unashindwa, utaendelea kushindwa zaidi na zaidi.
Uzuri ni kwamba, haijalishi ni kiwango gani cha ushindi, utaendelea kuvutia ushindi zaidi.
Hivyo muda wowote unaweza kuchagua kupata ushindi, na ukaendelea kupata ushindi zaidi.
Chagua ushindi mdogo mdogo, ambao utaelewa kwamba umeshinda, na hilo litavutia ushindi zaidi.
Kwa mfano chagua kuamka asubuhi na mapema, kuliko ulivyozoea kila siku na hata kama hujisikii, huu ni ushindi ambao unaweza kuutumia kushinda zaidi siku nzima.
Anza siku yako kwa kujisomea angalau kurasa chache za kitabu, ni ushindi mwingine mkubwa zaidi.
Weka dakika chache kwenye kuipangilia siku yako, na utakuwa unajiweka kwenye mazingira ya kushinda zaidi.
Fanya mazoezi na mwili utakuwa kwenye hali ya juu ya ushindi.
Ushindi unatengenezwa, kushindwa pia kunatengenezwa.
Chagua unatengeneza nini, na ukishaanza mengine yanajiendeleza yenyewe.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.