Kwenye maisha, huwa tunapata kile ambacho tupo tayari kukivumilia. Ndiyo maana unaweza kukuta mtu ana hali ngumu, na angeweza kuchukua hatua kuwa bora ila hafanyi hivyo kwa sababu anaweza kuvumilia hali hiyo ngumu. Angekuwa hawezi kuvumilia, angeshachukua hatua kuondokana na hali hiyo.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye biashara, biashara yetu inakua mpaka kufikia kiwango cha uvumilivu wetu. Hii ina maana kwamba, pale ambapo biashara yako ipo sasa, ndipo ambapo unaweza kupavumilia.
Hata kama inakuingizia kipato kidogo, basi angalau ni kipato ambacho unaweza kukivumilia, unaweza kukazana nacho na maisha yako yakaenda, hata kama ni kwa kujibana.

Kwa upande mwingine tunaweza kusema biashara yako itakua mpaka kufikia kiwango chako cha kutosheka. Yaani kama bado hujatosheka, kama ambavyo huwezi kuvumilia, utakazana kuweka juhudi kubwa katika kukuza biashara yako. Ukishafika hatua ambayo umetosheka, au unaweza kuvumilia, unaacha kuweka juhudi na unakuwa umefika kwenye kilele.
Sasa hii ni hatari sana kwa ukuaji wa biashara, kwa sababu kama tunavyoona, mabadiliko yanatokea kwa kasi kubwa. Watu wapya wanakuja na biashara zilizoboreshwa zaidi.
SOMA; BIASHARA LEO; Biashara Yako Inavyozidi Kukua, Unahitaji Kubadili Mikakati…
Kama wewe umeridhika au umefika hatua ya kuweza kuvumilia, hutadumu hapo kwa muda mrefu, utaishia kurudi nyuma, kwa sababu kadiri dunia inavyoenda mbele na wewe kubaki pale ulipo, unakuwa umechagua kurudi nyuma.
Kila siku unayokwenda kwenye biashara yako, jiulize ni kitu gani kipya unaweza kujaribu siku hiyo, hata kama ni kidogo kiasi gani. Kama huna cha kujaribu, jiulize kitu gani kipya unaweza kujifunza siku hiyo. Au panga kutembelea biashara yoyote, tofauti kabisa na ile unayofanya na jifunze watu wanaendeshaje biashara zao.
Usifikie hatua ya kuridhika haraka au kuvumilia chochote kwenye biashara yako, popote ulipo sasa, jua zipo hatua zaidi za kupiga. Siyo kwa lengo la kujidharau na kuona hujafanya kitu, bali kwa lengo la kuwa bora zaidi na kupiga hatua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog