Habari za leo rafiki yangu?

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio tunayotaka kwenye maisha yetu. Maisha ni mpango wa kutatua changamoto moja baada ya nyingine, hivyo unapokutana na changamoto usikate tamaa na kuona ndiyo mwisho wa safari yako. Bali jua hiyo ni hatua unayopaswa kupiga ili kuweza kufanikiwa.

Kwenye ushauri wa leo tutajifunza njia za kuweza kufaulu masomo pale unaposoma huku unafanya kazi au biashara. Pamoja na changamoto kubwa za mfumo rasmi wa elimu, bado mfumo huu ni muhimu hasa kufikia ndoto mbalimbali ambazo tunakuwa nazo.

Huenda unahitaji kupata utaalamu fulani, au kuongeza elimu yako ili kupata nafasi ya kufanya kitu fulani, zipo sababu nyingi zinazoweza kukupelekea uhitajike kurudi shuleni.

Changamoto kubwa inakuja pale ambapo unahitajika kusoma lakini wakati huo pia unafanya kazi au biashara. Hapo unakuwa na changamoto kubwa ya jinsi gani ya kupeleka vitu vyote kwa pamoja. Wengi wamekuwa wanashindwa na kujikuta wakiachana na masomo na kuona labda mpaka wakipata nafasi ya kutosha kusoma ndiyo watafanya hivyo.

Lakini mimi mara zote nimekuwa nakuambia kwamba unaweza kufanya vyote kwa pamoja, yaani unaweza kusoma na kufaulu vizuri, huku ukiwa unaendelea na kazi au biashara zako. Ni swala la kujipanga vizuri, kuwa na nidhamu kubwa na kujituma kwenye maeneo yote.

Kabla hatujaangalia njia gani utumie ili kufaulu pale unapokuwa unasoma huku una kazi au biashara, tusome maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili;

Habari kocha; Mimi ni mfanyakazi wa umma hapa Tanzania. Elimu Yangu ni kidato cha nne na nikasoma form six lakini awamu zote mbili nafeli. Naomba ushauri niachane na masuala ya kujiendeleza kimasomo nifanye kazi na biashara au nifanyeje? Maana ratiba za kazini zinanibana sana na nahisi ndiyo zinachangia kufeli kwangu. Anderson Y. M.

Kama alivyotushirikisha mwenzetu hapo, wapo watu wengi waliokwama kwenye hali kama hiyo. Ambapo kuendesha masomo na kazi au biashara linakuwa zoezi gumu na kufikia hatua ya kufikiria kuacha masomo kwa kuona hayawafai.

Nakwenda kumshauri Anderson hatua za kuchukua kwenye hali yake, na nina imani zitawasaidia wengine wengi pia.

Awali ya yote, kabla hatujaangalia ni hatua zipi za kuchukua, lazima kwanza ujiulize kwa nini umeamua kurudi shuleni kusoma, au kwa nini unapanga kufanya hivyo. Sababu zako za kurudi shule zinahitaji kuwa sahihi na zenye nguvu kama kweli utataka kupata kile unachotaka.

Kama unataka kurudi shule kwa sababu kila mtu ana elimu kubwa kuliko wewe, utaumia, kwa sababu kujitoa kunakohitajika kwenye kusoma huku ukifanya kazi, ni kukubwa na sababu ya wengine haiwezi kukupa nguvu ya kutosha.

Kama unataka kurudi shule, kwa sababu ukisoma mshahara wako utaongezwa, ni bora huo muda na gharama unazotumia kurudi shule ukaanzishe kitu kingine cha kukuingizia kipato kama biashara au hata uwekeze, kwa sababu ongezeko la kipato utakalopata kwa kuongeza elimu, halitaendana na juhudi ulizoweka au gharama ulizoingia.

Lakini kama umeamua kuongeza elimu ili kuwa bora zaidi wewe kama wewe, uweze kutoa thamani kubwa zaidi kupitia kazi na biashara yako, basi upo kwenye njia sahihi. Kwa sababu utaitumia elimu hiyo vizuri kuwa bora, na pia utapata msukumo mkubwa zaidi.

Sasa baada ya kupata sababu halisi ya kwa nini unarudi shule, na ukaamua kweli upo tayari kurudi shule wakati unaendelea na kazi au biashara yako, zingatia njia hizi tano ili kuweza kufanikiwa kwenye masomo na kazi zako pia.

  1. Jua kile unachopaswa kujifunza, unachopaswa kuelewa na unachoulizwa kwenye mtihani.

Usisome kwa mazoea au kwa sababu kitu fulani kimefundishwa au kuandikwa kwenye kitabu basi unakisoma. Badala yake soma kwa mkakati, jua kile unachopaswa kujifunza kwenye masomo unayofanya. Jua kile unachopaswa kuelewa, yaani baada ya masomo, inabidi uondoke na nini. Na muhimu zaidi jua kile utakachouliza kwenye mtihani.

Ni muhimu kujua vitu hivyo, ili muda na nguvu zako chache ulizonazo, uweze kuziweka eneo sahihi. Badala ya kupoteza muda na mambo mengi, unajua kwa kina yale muhimu na yatakayokuwezesha kuwa bora. Kwa kuwa kipimo kikuu cha kufaulu ni mtihani, basi maswali yanayoulizwa kwenye mtihani na namna unavyopaswa kuyajibu inapaswa kuwa kipaumbele kwako. Hata unaposoma, unajiuliza ni kwa namna gani unaweza kujibu swali kwa kile ulichosoma, na siyo usome tu kusema umesoma kitu fulani.

  1. Panga ratiba yako ya siku vizuri.

Kosa kubwa ambalo watu wengi wanaosoma huku wakifanya kazi au biashara wanafanya, ni kufikiri watapata muda wa kufanya vyote. Lakini wanakuja kustuka muda haupo kabisa. wanashangaa siku imeisha na hawajapata muda wa kusoma kama walivyofikiri wangepata.

Ukweli ni kwamba muda huwa haupatikani, muda huwa unatengwa, muda huwa unapangwa. Unahitaji kupanga ratiba yako ya siku ambayo inaonesha ni muda gani utafanya nini.

Katika ratiba hiyo, weka muda wa kusoma, KILA SIKU, ambao haupungui masaa matatu kwa siku. Na kila siku fuata ratiba hiyo. Unaweza kuanza kwa kuamka mapema na kupata muda wa kusoma, na pia kutumia muda wa mapumziko au muda baada ya kazi au biashara zao kusoma pia. Sehemu kubwa ya kujisomea ifanye muda wa asubuhi, ambapo akili bado haijachoka, utaweza kuelewa vizuri na kutumia muda mfupi.

  1. Usisome kwa kuzima moto.

Wanafunzi wote wana tabia moja, iwe ni mwanafunzi wa shule ya msingi, sekondari, au mwanafunzi wa chuo kikuu. Tabia hiyo ni kusoma pale mitihani inapokaribia. Wakati ambao siyo wa mtihani watu hutumia muda mwingi kwenye mambo mengine, lakini mtihani ukikaribia kila mtu anakuwa bize na kusoma. Hii inaitwa kusoma kwa kuzima moto.

Sasa wewe unayesoma huku unafanya kazi, usijaribu kabisa mtindo huo wa kusoma, lazima utafeli. Kwa sababu ambaye anasoma tu, anaweza kukesha siku tatu na kusoma vitu muhimu akajibu mtihani na kufaulu. Lakini wewe huna uwezo huo, una kazi zinakuhitaji kufanya pia. Hivyo anza kujiandaa na mtihani siku ya kwanza unapoanza kusoma. Jua mitihani inafanyika lini na mitihani inakuhitaji uwe umesoma mada zipi, kisha hakikisha unakuwa na ratiba ya kusoma kila siku ili umalize mada hizo kabla ya mtihani.

  1. Pata mtu wa kusoma naye, kujadiliana masomo mnayofanya.

Wakati mwingine kusoma wewe mwenyewe kunachosha, wakati mwingine unaweza kusoma lakini baadaye unagundua umesahau kila kitu. Ni hali ya kuumiza sana unaposoma. Kuondoa hilo, tafuta mtu mmoja au wawili ambao wanasoma kile unachosoma wewe, kisha kuweni na ratiba ya kusoma kwa pamoja na kujadiliana. Unaposoma na mtu mwingine, itakubidi ujisukume hata kama hujisikii kusoma. Na pia mnapojadiliana na wengine, unakumbuka zaidi kuliko kusoma mwenyewe. Unaweza kuwa kwenye mtihani, ukakutana na swali, halafu ukakumbuka mlijadiliana, au mlibishana kitu fulani.

Kupata watu mnaoelewana na mkasoma kwa pamoja itakusaidia sana. pia itakupunguzia mambo mengi ya kusoma kwa sababu mnaweza kugawana mada za kusoma halafu kila mtu akaja kumfundisha mwenzake, mnakuwa mmeua ndege wawili kwa jiwe moja.

  1. Soma kitabu PATA MASAA MAWILI YA ZIADA.

Kama hujasoma kitabu hichi basi unapaswa kukisoma. Kwa sababu hichi ni kitabu kitakachokusaidia wewe kupata muda wa kutosha kwenye siku yako kuweza kufanya kazi zako na kuendesha masomo yako. Niliandika kitabu hichi nikiwa nasoma masomo ya udaktari wa binadamu wakati pia nikiwa naendesha shughuli zangu nyingine kama uandishi na biashara.

Niliyokushirikisha ndani ya kitabu hicho ni yale niliyokuwa na ninayoendelea kufanya mimi ili kuhakikisha napata muda wa kutosha wa kufanya mambo yale muhimu.

Kitabu hicho kipo kwenye mfumo wa nakala tete (softcopy) na kinatumwa moja kwa moja kwenye email yako. Kupata kitabu hichi, tuma fedha tsh 5,000/= kwa simu 0755 953 887 au 0717 396 253 kisha tuma ujumbe wenye jina la kitabu, PATA MASAA MAWILI YA ZIADA, pamoja na email yako na utatumiwa kitabu hicho.

MASAA MAWILI YA ZIADA

Inawezekana kabisa kuendesha masomo na kufaulu huku ukifanya kazi au biashara zako. Unachohitaji ni kujitambua wewe mwenyewe na kujipanga vizuri ili kuweza kufanikiwa.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog