Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu USISUBIRI KUAMBIWA….

Dunia nzima ni kama inasubiri kuambiwa jinsi ya kufikiri, nini cha kufanya, jinsi gani ya kuishi, kipi cha kuvaa, kipi cha kula na kadhalika.

Utandawazi, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vimegeuka kuwa mashine kubwa ya propaganda ya kuwadhibiti watu.

Matangazo mbalimbali yameandaliwa kuwapeleka watu katika uelekeo fulani kwenye kufikiri na hata namna ya kuishi.

Hii ndiyo sababu watu wamekuwa wakikazana kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, hata kama hakina umuhimu kwao au siyo sahihi. Kwa sababu mashine hizi kubwa za propaganda, zinawafanya watu wanaotuzunguka ndiyo wawe washawishi wakubwa kwetu.

Ili kuondokana na hali hii, ili kuwa na uhuru na maisha yako, usisubiri kuambiwa kipi cha kufanya, jinsi gani ufikiri na namna gani uendeshe maisha yako.

Jua kipi unachotaka kwenye maisha yako, jua kipi upo hapa duniani kufanya, kisha fanya jambo sahihi, mara zote.

Hata kama hakuna mwingine anayefanya jambo sahihi, wewe fanya na utapata matokeo bora kabisa na maisha ya uhuru kwako.

Usiamke asubuhi na kusubiri dunia ikuambie unapaswa kujisikiaje siku hiyo, habari ipi ni muhimu na mafanikio ni nini. Amka ukiwa na mipango yako ya siku nzima, tengeneza habari zako mwenyewe na jua mafanikio kwako yana maana gani, kisha chukua hatua kuyafikia.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz