Tukichukua mfano wa shuleni, hata mtihani utungwe mgumu kiasi gani, wapo wanafunzi ambao watapata ufaulu mkubwa, na wapo ambao watapata ufaulu mdogo. Mtihani ukitungwa mrahisi pia, mambo yatakuwa hivyo hivyo, wapo watakaopata ufaulu mkubwa na wapo watakaopata ufaulu mdogo. Na kama ni darasa moja, mara nyingi wanaopata ufaulu mkubwa ni watu wale wale.
Kwenye kazi pia, hata kazi iwe ngumu kiasi gani, wapo watakaopata matokeo mazuri na wapo watakaopata matokeo ambayo siyo mazuri.
Ukweli ni kwamba, watu wanakaa ule upande ambao wanataka kukaa, kulingana na mapenzi yao, uwezo wao na hata kuridhika kwao.
Hata katika mambo ya kukubaliana, wapo ambao wanapenda kuwa upande wa kupinga. Chochote utakachosema wao wanakuwa na jambo la kupinga, au kuonesha kwa nini haifai.
Sasa kwa nini nakuambia hivi?
Kwa sababu tunaishi kwenye dunia ambayo tunapenda kumridhisha kila mtu. Tunapenda kuchukua hatua ambazo zitaleta matokeo sawa kwa kila mtu. Na tunapenda kufikia makubaliano ambayo kila mtu anakubali, hakuna anayepinga.
Hii ni hatari kwa sababu kama utatunga mtihani rahisi ili wale wanaopata ufaulu mdogo wapate ufaulu mkubwa, kumbuka wanaopata ufaulu mkubwa wataendelea kupata ufaulu huo. Kama utapunguza kazi ili yule anayechelewa kumaliza kazi amalize kwa wakati, kumbuka ataendelea kuchelewa kumaliza, na utakuwa umepunguza ufanisi kwa wale wanaomaliza kazi zao vizuri. Na kama unatafuta kujibu kila hoja ili asiwepo anayepinga, utajikuta kuna jambo jipya linaibuka la kupinga.
Ukweli ni kwamba watu wataendelea kukaa ule upande wanaotaka kukaa. Pamoja na juhudi utakazofanya kuwavuta wale wa chini kwenda juu, bado wataendelea kukaa chini katika juu mpya.
Pia kumbuka watu wengine wanapenda tu kupinga, kupinga mambo ndiyo kunawafanya wajisikie vizuri. Kila mtu anawategemea wapinge na hivyo hayo ndiyo maisha yao, kutaka kuhakikisha wanakubaliana na wewe bila ya upinzani wowote, ni kupoteza muda na nguvu zako bure.
Unapofanya kazi na watu wengine, unaposhirikiana na watu kwenye mambo mbalimbali, unapaswa kuelewa haya kwa kina, ili kuweza kutengeneza timu inayoelewa ubora na udhaifu wa kila mtu, na kuweza kuutumia kwa mafanikio ya kazi mnayofanya. Usitake kila mtu awe kwenye ngazi moja, akubaliane na kila kitu na aweze kufanya kama kila mtu anavyofanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
