Kumekuwa na changamoto kubwa kwenye kupata wasaidizi wa biashara wenye uwezo mzuri wa kufanya kazi kwenye biashara. Uaminifu na kujituma ni vitu ambavyo vinakosekana kwa wengi tunaowapata watusaidie kwenye biashara zetu.
Pamoja na changamoto kuwa kwenye tabia za watu, lakini sisi wamiliki wa biashara pia tuna mchango katika hilo. Kuna wakati sisi tunawafanya wasaidizi wetu washindwe kufanya kazi zao kwa ufasaha.

Kwa mfano kama usipomwelekeza msaidizi wako vizuri kuhusu majukumu yake, na matokeo gani anategemea kuzalisha, hataweza kufanya kazi yake kwa ufasaha. Atajitahidi kufanya vile anavyoweza yeye kwa sababu hana mwongozo sahihi.
Sasa katika kuwawezesha wasaidizi wako kufanya kazi vizuri, lipo swali moja muhimu sana ambalo wanapaswa kuweza kulijibu kwa ufasaha. Wewe ndiye unayepaswa kuwasaidia kupata jibu la swali hili, ila watapaswa kuliishi jibu hilo kila siku.
Swali lenyewe ni je kile ninachofanya kila siku kwenye biashara kinamsaidiaje mteja wa biashara hii?
Hili swali lazima kila mtu anayehusika kwenye biashara yako aweze kulijibu kwa usahihi. Lazima aweze kuona kile anachofanya, kinamgusaje mteja moja kwa moja. Hata kama siyo yeye anayemhudumia mteja, anapaswa kujua kile anachofanya, kinahusikaje katika kuhakikisha mteja anapata kitu bora kabisa, kile ambacho anakitaka.
SOMA; BIASHARA LEO; Katika Mipango Yako Ya Biashara, Mteja Ni Sehemu Muhimu…
Kama msaidizi wako hawezi kujibu swali hilo la kwamba anachofanya kinamsaidiaje mteja, labda wewe hujamwelewesha vizuri majukumu yake na umuhimu wa majukumu hayo, au yeye mwenyewe hazingatii wajibu wake. Kwa yote hayo, lazima wewe kama mmiliki wa biashara ujali na kuhakikisha wasaidizi wako wanawawezesha wateja kupata kile wanachotaka.
Kumbuka wateja ndiyo wanaifanya biashara yako iendelee kuwepo, ndiyo wanakufanya wewe uweze kuendesha maisha yako. Hivyo chochote unachofanya, mteja anapaswa kuwa namba moja.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog