It is not death that a man should fear, but he should fear never beginning to live. – Marcus Aurelius
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nzuri na ya kipekee sana ya leo.
Ni nafasi bora kwetu ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya nakubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JE UMESHAANZA KUISHI?
Kama kipo kitu kimoja ambacho watu wanakihofia sana, basi ni kifo.
Watu wamekuwa wanatishwa na kifo, wamekuwa wanapata hofu kubwa kila wakifikiri kuhusu kifo.
Lakini cha kushangaza kabisa ni kwamba, watu hao wanaohofia kifo, hawajaanza hata kuishi maisha yao.
Ni watu wa kuahirisha kila wakati kuyaanza maisha yao, wakitaka kufanya kitu wanasema mpaka kitu fulani kikae sawa.
Wanajiambia wakishamaliza kitu fulani basi wataanza maisha yao.
Kuhofia kifo, ni jambo la ajabu na la kupoteza muda kwa sababu historia inaonesha hakuna mtu amewahi kuondoka hapa duniani akiwa hai.
Kifo ni njia ya kila mmoja wetu.
Hivyo badala ya kuweka muda wako kwenye kufikiri kuhusu kifo, hebu weka muda huo kwenye kuanza kuishi maisha yako.
Kuishi yale maisha ya uhalisia kwako, yale maisha ambayo yana maana kwako na mchango kwa wengine.
Ukiishi maisha yako, huna haja ya kuhofia kifo. Kwa sababu kwa wakati wowote, utakuwa unafanya jambo sahihi kwako.
Ishi maisha yako leo, ishi maisha yako kila siku, usiahirishe na kusema utaanza kuishi baada ya kukamilisha vitu fulani. Muda wa kuishi maisha yako ni sasa.
Uwe na siku bora na ya kipekee sana leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa