Dunia imekuwa inawadanganya watu kitu kimoja, kwamba ipo njia ya kukimbia
ugumu, ipo njia nyepesi na ambayo haina changamoto wala ugumu wowote.
Ukiwa kwenye njia hiyo, wewe ni kwenda tu, hakuna cha kukusumbua.
Na watu wanajaribu njia hizo, zinafanya kazi kweli, kweli ugumu unaondoka,
inakuwa kama ni maajabu. Wakati wengine wanakazana na ugumu, wao
wanakuwa kwenye ulaini, mambo mazuri.
Ni mpaka baadaye, mambo yanapokuja kubadilika ndipo wanagundua kwamba
hawakuwahi kuukimbia ugumu, waliusogeza tu mbele. Waliuhamisha kwa
muda, lakini wamekuja kukutana nao tena.
Chukua mfano wa watu wawili, wote wameanza kazi au biashara kwa wakati
mmoja na kwa hali sawa. Mmoja anatumia kipato chake, kwa kujipa maisha
anayoyataka, hataki shida. Mwingine anajibana, anaweka akiba na kukuza
biashara yake. Baada ya miaka kumi, aliyekuwa anajipa raha atakavyo,
anakuwa yupo kwenye wakati mgumu huku aliyekuwa akijinyima akiwa
kwenye wakati mzuri.

Unaweza pia kuchukua mfano wa mtu anayeendesha biashara yake kwa njia za
kona kona, ambaye kuna mambo anayafanya ambayo ni kinyume na sheria, ila
anapata faida kubwa. Wakati huo huo yupo mfanyabiashara mwingine
anayeendesha biashara yake kwa uadilifu, hapati faida kubwa na mambo
yanaonekana magumu kwake. Baada ya muda, yule wa kona kona anakutana
na mkono wa sheria na hawezi kuendelea tena. Ila yule aliyekuwa akiendesha
kwa uadilifu, anakuwa anaendelea na bi
Popote unaposhawishika kupita njia ya mkato, unaposhawishiwa kwamba
unaweza kuondokana na ugumu kabisa, jiulize kwa makini, je ugumu huo
unauhamishia wapi?
SOMA, #UKURASA WA 1027; Matokeo Na Mchakato, Wakati Sahihi Kwa Kila Kimoja….
Na nakushauri sana rafiki yangu, ni vyema kupambana na ugumu sasa kuliko
siku za mbeleni. Kwa sababu ugumu unaokuja mbeleni, unakatisha tamaa, hasa
pale unapokuwa umepitia kipindi ulichokuwa unaona ni kizuri kwako.
Hukimbii ugumu, unauhamisha. Jiulize na kutafakari hilo kwa kila hatua
unayochukua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea
http://www.mtaalamu.net/patablog