It is not the man who has too little, but the man who craves more, that is poor. – Lucius Annaeus Seneca
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya nakubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UMASIKINI NI KUTOKURIDHIKA.
Kuna watu ambao hawana mali nyingi sana, lakini maisha yao ni bora na ya furaha sana.
Na wapo watu ambao wana mali nyingi mno, lakini bado hawana furaha na kuona bado kipo walichokosa.
Katika makundi hayo mawili ya watu, wale wenye mali lakini hawana furaha ndiyo masikini wakubwa kuliko wasiokuwa na mali.
Unasikini siyo tu kukosa mali au fedha, bali hali ya mtu anapokuwa au asipokuwa na fedha.
Wale wasioridhika na kushukuru kwa kile walichonacho, wanaendelea kuwa masikini hata wawe na mali nyingi kiasi gani.
Hivyo ni muhimu sana kuridhika, ni muhimu kushukuru kwa kila hatua unayopiga, na ni muhimu kuthamini kila ulichonacho. Hata kama siyo ulichotegemea au unachotaka, kushukuru kunavutia vingine vingi zaidi.
Vunja mzizi mkuu wa umasikini ambao ni kutokuridhika na kutokushukuru na anza kushukuru kwa kila ulichonacho sasa na huu utakuwa mlango wa utajiri kwako.
Uwe na siku njema sana leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa