Kuna nyakati kwenye maisha utajikuta njia panda, ambapo kuna mengi ya
kufanya lakini hujui ufanye lipi. Na huenda ukawa unategemea ushauri kutoka
kwa watu fulani ambao nao huwapati kwa ajili ya ushauri. Hapo ndipo wengi
wanapokwama, wakiogopa kufanya maamuzi kwa kuhofia kukosea au kukosa
fursa nzuri.
Kitu muhimu kabisa katika nyakati kama hizo, ni kufanya kilicho sahihi. Kwenye
kila hali ambayo mtu unapitia, kipo kitu sahihi cha kufanya. Hata kama siyo
kilicho bora kufanya, lakini kwa hali unayokuwa nayo kinakuwa ndiyo kitu
sahihi. Fanya hicho.
Unapofanya kitu sahihi haimaanishi ndiyo kitakuwa bora, bali ni hatua ya
kwanza. Utaendelea tena kufanya kilicho sahihi mara kwa mara. Hii ina maana
kwamba ukifanya kilicho sahihi sasa siyo kwamba umeshamaliza, bali utahitaji
kuendelea kufanya, kila siku.


Unapofanya kitu sahihi kwenye hali uliyokuwa njia panda, haimaanishi
kitakuwa bora sana, lakini itakuwa njia nzuri ya kuanza kwa sababu baada ya
hapo utaendelea kufanya kilicho sahihi. Hivyo kama ulikosea, au ulichodhani ni
sahihi hakikuwa sahihi, unapogundua unafanya kilicho sahihi.
Sijui unaona hapo rafiki yangu, kwamba huhitaji kukwama wala kuogopa
kufanya maamuzi kwa sababu utakosea. Badala yake fikiria kipi ni sahihi kwa
wakati huo, kifanye. Unapokuja kugundua kwamba ulichofikiri siyo sahihi, hapo
hapo unachukua hatua ya kufanya kilicho sahihi.

SOMA, # Ukurasa Wa 1027; Matokeo Na Mchakato, Wakati Sahihi Kwa Kila Kimoja….

Hivyo ni muhimu sana ufanye kilicho sahihi kila mara, na kuendelea kujiuliza
yale uliyofanya ndiyo sahihi kabisa? kama utapata taarifa mpya, kama utapata
maarifa mapya, kama utapata uelewa mpya na kugundua ulichofikiri ni sahihi
mwanzo siyo sahihi, usipoteze muda kujilaumu au kuona umepotea, fanya
kilicho sahihi.
Huu ni msingi mzuri sana kuishi, haimaanishi hutakosea, badala yake utakua na
kuwa bora zaidi kila siku, kwa sababu unafanya kilicho sahihi mara zote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea
http://www.mtaalamu.net/patablog