Tofauti kubwa kabisa ambayo sisi binadamu tunayo na viumbe wengine wowote ni utashi wetu, ambao unatuwezesha kufanya maamuzi sahihi kulingana na hali ambayo tunapitia. Hichi ni kitu kikubwa ambacho kinatupa sisi binadamu uwezo wa kutawala viumbe wengine.
Lakini cha kushangaza, wengi wetu tumekuwa hatutumii uwezo huu mkubwa sana uliopo ndani yetu. Tumekuwa tunataka kukaa kama viumbe wengine, kukaa pale tulipo na kila kitu kitokee pale pale, kama hakipatikani basi tutalalamika na kulaumu wengine, lakini hatutachukua.

Kwa mfano, mtu ambaye yupo kwenye kazi ambayo haipendi, na kila siku anailalamikia, lakini haondoki, anaendelea kuwa kwenye kazi hiyo, hapigi hatua yoyote, ana tofauti gani na mti ambao umeoteshwa sehemu isiyo na maji na hivyo kudumaa?
Ni hivyo, mti ukiwa kwenye mazingira magumu, utakazana kurefusha mizizi yake ili kufikia maji yaliyopo mbali, lakini wenyewe hauwezi kuondoka pale ulipo. Hivyo mti utapambana pale ulipo, japo hakuna matumaini ya matokeo makubwa.
Sasa na wewe unapochukua hatua kama za mti, wakati zipo hatua bora kabisa unaweza kuchukua, utashindwa kujitofautisha na mti.
Unajua kabisa wewe siyo mti, unajua una uwezo wa kufikiri, wa kuona vitu kwa njia tofauti. Lakini hutumii uwezo huo, unataka kuwa kama mti, kila kitu kitokee hapo ulipo, usichukue hatua yoyote.
SOMA; UKURASA WA 1006; Kutaka Kupata Na Kuepuka Kupoteza…
Kwa kufanya hivyo hujitendei haki, unajinyima mambo mazuri ambayo yangeweza kutokea kama tu ungechukua hatua. Kama ungeanza kujishughulisha na mambo mengine, kuacha yale yanayokukwamisha.
Rafiki yangu wewe siyo mti, kama kuna sehemu upo na haikuridhishi, usilalamike na kuendelea kuwa pale, badala yake chukua hatua, chukua hatua hata ndogo ndogo, na baada ya muda zitaleta matunda makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog