Kitu kigumu kwa wengi huwa kimekuwa ni kuingia kwenye biashara. Wengi wanapata shida wakati wa kuchagua biashara gani wafanye na wapate wapi mtaji. Wakishavuka hatua hiyo na kuweza kuanza biashara, wengi huishia hapo.
Biashara zao zinabaki kwenye ngazi ile ile ambayo walianzia na hazikui zaidi. Wanaendesha biashara zao kwa mazoea na wanabaki pale pale. Miaka inaenda na mtu anakuwa kwenye ngazi ile ile kibiashara.
Kama ni duka basi linakuwa duka moja, kama ni huduma basi inakuwa ni ile ile, wateja wale wale na kinachofanyika ni kile kile.

Hili huwa ni hatari sana kibiashara kwa ngazi mbili, moja ni mabadiliko kuiacha biashara nyuma. Hapa mambo yanabadilika kiasi kwamba biashara inakuwa haina tena soko au uhitaji. Mbili ni ushindani, watu wanakuwa wanajua kile unachofanya na kukuiga, na wakaweza kuboresha zaidi na hivyo kuweza kukuchukulia wateja wako.
Kuepuka hayo, biashara inapaswa kuwa na hatua. Isitokee hata siku moja ukaona biashara yako imefikia kilele. Kuwa na hatua zaidi unazotaka kupiga kupitia biashara yako. Kama unaanza na duka moja, kuwa na wazo la kuwa na maduka mengi zaidi. Kama unaanza huduma na watu wachache, panga kuwafikia watu wengi zaidi.
SOMA; BIASHARA LEO; Ushauri Bora Kabisa Wa Biashara Yako Upo Kwenye Tabia Za Wateja Wako…
Popote unapoanzia na biashara yako, popote pale biashara yako ilipo sasa, usione kama ndiyo mwisho, bali ona ni mwanzo wa safari ndefu sana kwako kibiashara.
Tengeneza hatua zaidi, wenga ngazi za kupanda kibiashara, fikia wateja wengi zaidi, fika maeneo mengi zaidi na endelea kuboresha zaidi. Dunia tunayoishi sasa, chochote ambacho hakibadiliki, kinapotezwa kabisa.
Badili biashara yako, piga hatua zaidi, kila siku.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog