You must live for another if you wish to live for yourself. – Lucius Annaeus Seneca
Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Ni siku nyingine nzuri na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili tuweze kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya nakubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUISHI KWA AJILI YAKO….
Kwa sehemu kubwa, sisi binadamu ni wabinafsi. Tunajali mambo yetu zaidi ya mambo ya wengine.
Japo siyo kitu kibaya kufanya hivyo, kuna kiasi ambacho lazima kiangaliwe.
Na kama kweli unataka kujali mambo yako, hatua muhimu kabisa ni kuanza kujali mambo ya wengine.
Kama unataka kuishi kwa ajili yako, basi ishi kwa ajili ya wengine.
Unapoishi kwa ajili ya wengine, moja kwa moja unaishi kwa ajili yako.
Unapoweka juhudi za ziada kuhakikisha maisha ya wengine yanakuwa bora, maisha yako yanakuwa bora zaidi.
Chochote unachotaka kwa ajili yako, anza kukifanya kwa ajili ya wengine, anza kukitoa kwa wengine.
Uwepo wetu hapa duniani ni kwa ajili ya wengine.
Na chochote tunachotaka, kinatoka kwa wengine.
Chochote unachofanya, angalia wengine wananufaikaje na kile unachofanya.
Uwe na siku bora sana leo rafiki, siku ambayo kila anayekutana na wewe, anakuwa bora zaidi.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa