Kila siku kuna magari mengi yanafanya safari zake na yanafika salama. Hutasikia yakitangazwa kama magari kadhaa yalifanya safari leo na kufika salama. Lakini ikitokea gari moja limepata ajali, basi kila mtu atajua, itatangazwa na kusambazwa mno. Hili ni gari moja kati ya maelfu ya magari yaliyofanya safari siku hiyo.
Ukifanya mambo mazuri, hutasikia watu wakizungumzia kuhusu wewe, wengi watakaa kimya, wengine hawatajua hata kama upo. Lakini utakapofanya jambo moja baya, kila mtu atajua kuhusu jambo hilo na kuhusu wewe. hilo baya ulilofanya litasambaa na kuwafikia wengi.
Watu wanaofanya mabaya wanajulikana zaidi kuliko wale wanaofanya mambo mazuri. Na mambo mabaya yanavutia umbeya zaidi kuliko mambo mazuri.

Wapo watu wengi ambao hawakuwa wakijulikana kabisa, walikuwa wanaendelea na maisha yao bila ya bugudha yoyote, lakini walipofanya makosa, kila mtu aliwajua na maisha yao yakaanza kuwa na bugudha za kila aina.
Kwa nini nakuambia haya?
Kadiri unapofanikiwa, ndivyo kosa dogo unaloweza kufanya linaweza kuharibu kabisa maisha yako na mafanikio yako. Utafanya mazuri mengi mno ambayo watu wanayachukulia kawaida. Lakini utafanya baya moja na litafuta kila zuri ambalo umewahi kufanya.
Hivyo ni wajibu wetu sisi wanamafanikio, kuhakikisha tunaishi kwa misingi ambayo itatuepusha kufanya makosa ambayo yatatuharibia zaidi. Na hili halianzi baada ya kuwa umefanikiwa, bali linaanza kabla hata hujafanikiwa. Kuna mambo unaweza kuwa ulikuwa unayafanya zamani, na watu wakaja kuyafukua baada ya wewe kufanikiwa.
SOMA; UKURASA WA 441; Dunia Inakusoma Tu…
Hiyo ndiyo dunia, ielewe na endesha maisha yako kwa njia ambayo utaepuka misuguano isiyo ya muhimu.
Kama ambavyo nimekuwa nasema, tunaishi kwenye dunia ambayo kitu siri hakipo tena. Kila kitu kipo wazi na chochote unachofanya, dunia nzima ina uwezo wa kujua. Utaongea kwenye simu na mtu ukiamini ni siri kumbe yeye anakurekodi. Utafanya kitu ukijua ni kidogo kumbe watu wanapiga picha na kuchukua video. Ushahidi utakuwa kila mahali na kama ni jambo baya, litakuharibia sana.
Ishi kwa misingi ambayo itakuwezesha kufanya mambo sahihi nyakati zote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog