We are more often frightened than hurt; and we suffer more from imagination than from reality. – Lucius Annaeus Seneca

Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Nafasi hii ya kipekee tuliyoipata leo, tunapaswa kuitumia vyema ili tuweze kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya nakubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UNAJITESA ZAIDI YA UNAVYOTESWA…
Fikra zetu zina nguvu kubwa sana kwetu,
Kile tunachofikiri, kinaweza kutuumiza zaidi ya kitu chenyewe.
Kwa mfano, hofu ya kushindwa, itakuumiza zaidi ya kushindwa kwenyewe.
Kwa sababu mambo mengi unayohofia, hayatatokea kabisa. Lakini hofu inakuwa kubwa na inayoweza kukuumiza.

Mtu akikujibu vibaya, au akafanya kitu ambacho ni kibaya kwako, na wewe ukaendelea kuwa na kinyongo naye, unakuwa unaendelea kujitesa zaidi. Mtu alifanya kitu cha kukuumiza mara moja, wewe unaendelea kujiumiza kila siku, wakati huo huenda yeye alishasahau kabisa.

Kuepuka hali hii ya kujitesa mwenyewe, kwanza kabisa usikubali hofu yoyote ikutawale. Unapokuwa na hofu juu ya jambo lolote, chukua hatua, utagundua kwamba mengi unayohofia wala hayatokei.

Iwapo mtu amefanya kitu cha kukuumiza au kukukera, malizana naye mapema kabisa. Labda msamehe na achana naye, au mkabili na kumweleza alichokifanya hakijakupendeza, na ukishamalizana naye mambo hayo yaishie hapo.
Kuendelea kufikiria mambo hayo kwa muda mrefu, utajitesa bila ya maana yoyote.

Usikubali kuendelea kujitesa, jipe uhuru, jipe sababu ya kuwa na amani wakati wote.
Kafute mateso yote ya kujitakia leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa