KITABU; How to Think Like Leonardo da Vinci / Michael J. Gelb
UKURASA; 154 – 163.
Leonardo aliwahi kusema kwamba KILA KITU KIPO NDANI YA KILA KITU, KINATOKA NDANI YA KILA KITU NA KINARUDI KWENYE KILA KITU.
Kauli hii ilimaanisha kwamba, dunia imeungana na dunia ni kitu kimoja.
Kila kitu hapa duniani ni kitu kimoja, viumbe wote hapa duniani tumeunganishwa na kuwa kitu kimoja.
Maisha na uhai hapa duniani ni kitu kimoja.
Leornado anatuambia pia ya kwamba, dunia ipo ndani yetu ma sisi tupo ndani ya dunia. Ukiangalia miili yetu ni sawa na dunia.
Mifupa inaifanya miili yetu kuwa imara, miamba inaifanya dunia kuwa imara.
Ndani yetu tuna kimiminika kikuu ambacho ni mzunguko wa damu, unaofanya maisha yetu yaweze kwenda. Maisha ya dunia yanaendeshwa na kimiminika kikuu ambacho ni maji.
Mishipa ya damu inasambaza damu mwilini, mito na vijito vinasambaza maji duniani.
Kufahamu umoja wetu na dunia na kila kilichopo ndani ya dunia, kunatuwezesha kujua utegemezi wetu kwa kila kitu kilichopo hapa duniani. Pia madhara tunayoweza kusababishia wengine hapa duniani.
Kwa kuwa sisi ni dunia na dunia ni sisi, kuiharibu dunia ni kujiharibu wenyewe na kujiharibu wenyewe ni kuiharibu dunia.
Hivyo kama unajipenda mwenyewe au unaipenda dunia, ishi maisha mazuri kwako, kwa wengine na kwa dunia pia.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa