KITABU; Meditations / Marcus Aurelius.
UKURASA; 1 – 10.

Marcus Aurelius, aliyekuwa mtawala wa Roma kati ya mwaka 161 mpaka kifo chake mwaka 180 anaandikwa kama mmoja wa watawala watano bora kabisa wa Utawala Wa Roma.
Marcus alizaliwa katika familia ya kawaida na baada ya wazazi wake wake kufariki aliasiliwa na familia ya watawala wa Roma.

Tangu akiwa mdogo Marcus alipata elimu bora na pia alipata elimu ya falsafa ya ustoa. Aliipenda falsafa hii na aliishi kwa matendo.
Baada ya baba aliyemuasili kufa, alikuwa mtawala wa Roma akisaidiana na mdogo wake ambaye pia aliasiliwa.

Kipindi cha utawala wa Marcus kilikuwa kipindi kigumu sana kwa Roma. Palikuwa na vita nyingi za kupigana, ambazo Marcus alipigana mstari wa mbele. Hakukaa tu kuagiza wanajeshi wapigane, bali yeye mwenyewe alisafiri na kwenda kwenye vita hizo.
Pia ilitokea njaa kubwa katika kipindi cha utawala wake.

Pamoja na changamoto hizo, Marcus aliweza kuiongoza vizuri Roma na kuifanya kuwa imara zaidi.
Moja ya vitu vulivyomsaidia sana katika uongozi wake na maisha yake ni falsafa ya ustoa.

Kitabu cha Meditations, ambacho kimeandikwa na Marcus Aurelius, hakikuandikwa ili kuwa kitabu, bali kiligundulika baada ya Marcus kuwa amefariki.
Yaliyomo kwenye kitabu hichi, ambayo ni mazuri mno kwa kuwa na maisha bora, hayakuandikwa kwa ajili ya wengine, bali Marcus aliyaandika kwa ajili yake mwenyewe.

Marcua alikuwa na kitabu (journal) ambacho kila siku alikiandika, kila siku aliandika yale aliyojifunza, yale aliyofanya na yale aliyokosea.
Kupitia kitabu hichi, tutajifunza mengi sana kwa namna Marcus alivyoweza kuendesha maisha yake katika nyakati ngumu.

Marcus pia anasemwa kama mmoja wa wanafalsafa wa ustoa ambao walikuwa wakubwa. Ukubwa wake kwenye falsafa unatokana na jinsi alivyoiishi, na wala siyo kuihubiri au kuifundisha kwa wengine. Licha ya kuwa mtawala wa Roma, hakuwahi kuwalazimisha watu wakubali na kuishi falsafa aliyoishi yeye ya ustoa. Badala yake alimkubali kila mtu kwa falsafa yake na yeye kuishi falfasa yake.

Karibu kwenye safari hii ya #KURASA_KUMI ZA KITABU tujifunze kupitia kitabu cha Meditations cha Marcus Aurelius.

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa