The best revenge is to be unlike him who performed the injury. – Marcus Aurelius

Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari NJIA BORA YA KULIPA KISASI…
Kwenye maisha wapo watu wanaofanya vitu ambavyo vinakuumiza, kukuudhi au kukukatisha tamaa.
Watu hao wanaweza kuwa wanajua wanachofanya au hawajui.

Kutokana na mambo hayo ambayo watu wanakuwa wamekufanyia, yanashawishi sana mtu ulipe kisasi. Unashawishika sana kifanya kitu ili kuwafundisha somo watu hao, nao wajue kwamba wanayofsnya siyo mazuri.

Lakini kitu chochote unachofanya, ambacho kinafanana na kile walichofanya wao kinakufanya na wewe uwe kama wao.
Yaani kama mtu amekuumiza na wewe ukalipa kisasi kwa kumuumiza, basi wote mnakuwa hamna tofauti. Wote mnakuwa waumizaji.

Njia bora kabisa kwako ya kulipa kisasi, ni kutokuwa kama yule ambaye amekufanyia kitu.
Kama mtu amekuumiza basi wewe humuumizi, badala yake unafanya lililo jema kwake.
Kama mtu amekudharau basi wewe unamheshimu.
Kwa kufanya hivi, utakuwa umeepuka kuwa kama yeye na hivyo kuacha kufanya mambo kuwa magumu na makubwa.

Kumbuka, hufanyi hivyo kutaka kumwonesha au kumfundisha chochote, bali unafanya hivyo kwa sababu zako binafsi. Unafanua hivyo kwa sababu hutaki kuwa kama yeye, hutaki kuishia kama yeye, kuwa mtu unayefanya mambo yasiyofaa kwa wengine.

Lipa kisasi kwa kukataa kuwa kama yule aliyekufanyia ubaya wa aina yoyote.
Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha