You are a little soul carrying around a corpse. – Epictetus

Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari ROHO ILIYOBEBA MWILI…
Sisi binadamu ni viumbe wa kiroho ambao tumebeba mwili.
Na siyo kama wengi wanavyofikiri kwamba sisi ni viumbe wa kimwili ambao tumebeba roho.

Ukifikiria kwamba wewe ni kiumbe wa kimwili, utakazana na mwili, ambao mwisho wa siku hautakuridhisha kwa namna yoyote ile. Utazidi kutaka zaidi chochote ambacho kinaufurahisha mwili, na mwishowe unakuwa mteja wa kile unachokazana nacho kwenye mwili.

Lakini unapojichukulia kwamba wewe ni kiumbe wa kiroho ambaye umebeba mwili, kipaumbele chako kikubwa kitakuwa kwenye roho, kwenye imani yako. Utajijenga kuwa imara kwenye upande wa roho na hilo litakuwezesha kuwa na maisha bora na yenye furaha ya kudumu.

Changamoto ni kwamba kuufanyia kazi mwili ni rahisi kuliko kuifanyia kazi roho. Mwili una tamaa nyingi ambazo usipoweza kuzidhibiti roho itaanguka.
Hivyo weka mkazo sahihi kwenye eneo sahihi kwako ambalo ni roho.

Kama alivyosema Epictetus, siyo tu kwamba wewe ni kiumbe wa kiroho uliyebeba mwili, bali wewe ni roho ndogo iliyobeba maiti.
Kazana kukua na kukomaa kiroho, maisha yako yatakuwa bora sana.

Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha