Sometimes even to live is an act of courage. – Lucius Annaeus Seneca
Asubuhi njema kwako rafiki yangu.
Hongera kwa nafasi hii ya kipekee, nafasi ambayo tunakwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUNA WAKATI HATA KUISHI NI UJASIRI….
Kwenye maisha yetu, tunapitia hatua mbalimbali.
Kuna wakati mambo yanaenda vizuri na tunakuwa na matumaini makubwa.
Lakini pia kuna wakati ambapo kila kitu hakiendi na tunaelekea kukata tamaa.
Kuna wakati hata kuishi tu inakuwa ni ujasiri mkubwa. Huu ni wakati ambapo kila kitu kinaonekana kukwama, mbele linaonekana giza na kila tumaini ambalo mtu unalo linazimika mbele yako.
Wakati kama huu ndiyo unaojenga maana ya maisha yako, ndiyo wakati ambao unajifunza na kuweza kuchukua hatua kubwa za kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.
Usikubali kabisa kukata tamaa, hata kama kila ulichokuwa unategemea kimekuangusha. Kama bado unapumua, bado unayo nafasi, muhimu ni kuendelea kufanya kilicho sahihi, kwa pale ulipo.
Kila kitu kina mwisho wake, hivyo hata magumu na changamoto, kuna wakati yatafikia mwisho.
Endelea na ujasiri wako katika kuishi, na ishi kila dakika ya maisha yako kwa ujasiri wa hali ya juu.
Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha