Nataka kuanza biashara lakini bado sijajiandaa vya kutosha….

Nasubiri mpaka niwe tayari ndiyo nianze kufanya…

Nataka kuandika lakini bado sijajifunza vya kutosha…

Nataka kuboresha zaidi kazi zangu lakini kwa sasa bado sijakamilika…

Zote hizo ni dalili za kujificha. Unataka kufanya kitu, lakini unajificha kwenye sababu fulani, ambazo zinaweza kuwa kweli au siyo kweli.

Kila Mtu

Kwenye mafanikio, kuna kufanya au kujificha.

Kujificha ni pale ambapo una kila sababu kwa nini huwezi kufanya kitu. Sababu hizo tunaziita kujificha kwa sababu hakuna mtu atakayekuona kama hutafanya. Umeamua kujificha, na hakuna atakayekuona au kukusumbua.

Kufanya ni pale ambapo unachukua hatua ya kupiga hatua fulani, unaleta kitu katika uhalisia, kitu ambacho kinaonekana na watu, kitu ambacho kinaweza kuwasaidia watu.

Kujificha ni rahisi, haihitaji nguvu wala uthubutu wowote. Ni wewe kuwa tu na sababu halafu ukajiaminisha hivyo. Pia ukijificha hakuna anayeweza kukusumbua, ila pia huwezi kufanikiwa.

SOMA; UKURASA WA 757; Nenda Kinyume Na Sababu Ulizonazo, Leo Tu…

Kufanya, kuonekana ni kugumu. Kwanza kabisa kuna uwezekano wa kushindwa, pamoja na kuwa na mipango mizuri, ipo nafasi ya kushindwa. Na ukishindwa unaonekana na wengi kwamba umeshindwa. Hii ndiyo sababu wengi wanaogopa kufanya na kuonekana.

Swali ni je wewe unajificha wapi? Ni sababu gani unayojipa wewe ya kutokufanya sasa? Ni kipi unajiambia kwamba utafanya baada ya kuwa tayari?

Wito wangu kwako, acha kujificha, jitokeze hadharani, fanya kitu ambacho kinaweza kushindwa na hatimaye utafanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog