Hakuna kitu ambacho huwa kinanishangaza kama uharaka wa watu kutaka mafanikio bila ya kuwa na subira. Watu hufikiri kwamba kwa sababu wameshajua nini wanataka, kwa sababu wameshaweka malengo, kwa sababu wameshakuwa chanya na wanaweka juhudi, basi wanapaswa kupata matokeo hapo hapo.
Lakini hebu tuiangalie asili katika uzalishaji. Hakuna kiumbe ambacho kinazaliwa na chenyewe kuanza kuzaa hapo hapo. Kuna muda unahitajika, maandalizi yanahitajika, ukomavu pia ili kuweza kuzalisha.

Mtoto mdogo hawezi kubeba au kusababisha ujauzito na uzalishaji ukafanyika salama. Kadhalika mti wa mwembe hautaota leo na kuanza kutoa maembe hapo kwa hapo. Unahitaji muda wa kukomaa, ili hata kuweza kubeba hiyo miembe ambao itazalishwa.
Kadhalika kwenye mafanikio yetu pia, unahitaji maandalizi na ukomavu wa kuweza kustahimili kiwango cha mafanikio utakachopata.
Nadhani umewahi kuona watu ambao walipata mafanikio makubwa bila ya maandalizi ya kutosha ya kuwa na ukomavu wa kuhimili mafanikio hayo. Labda ni mtu ameshinda bahati nasibu au kurithi mali nyingi. Huenda pia mtu amekutana na nafasi nzuri ambayo ingemwezesha kupiga hatua kubwa.
SOMA; UKURASA WA 796; Changamoto Kuu Ya Sasa Ni Subira….
Lakini mtu huyo anachezea nafasi hiyo na kuipoteza. Watu kwa nje wanashangaa inakuwaje mtu anachezea nafasi nzuri kama hiyo. Kumbe yeye mwenyewe ndani yake hajui hata kwa nini anachezea nafasi hiyo. Yeye mwenyewe anakuwa anashangaa namna mambo yanavyoenda kasi.
Hii inatokana na kukosa ukomavu wa kuweza kustahimili kiwango hicho cha mafanikio. Ni sawa na mtoto kubeba mimba kabla ya muda wake, ikapelekea mimba hiyo kutoka au hata yeye kupoteza maisha.
Mara zote jua kuna muda unahitajika kwako kujiandaa na kukomaa kwa ajili ya mafanikio makubwa yanayokuja. Muhimu ni wewe kuweka juhudi kubwa kuhakikisha unakuwa bora zaidi kila wakati, pamoja na kuweka juhudi zaidi.
Acha na dunia iliyovurugwa, dunia ambayo watu wanataka kitu na wanakitaka sasa, hawana subira. Haishangazi wanapopata wanachotaka kinakuwa angamizo kwao.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog