Moja ya tabia ambazo ni sumu kwa mafanikio ya wengi ni tabia ya kuahirisha mambo. Mtu unakuwa na hamasa kubwa ya kupiga hatua kwenye maisha yako, unaweka malengo na mipango na unajua kabisa nini unapaswa kufanya ili kufika pale unapotaka kufika.

Lakini changamoto inakuja pale unapofika wakati wa kufanya. Hapa ndipo sababu nyingi zinapojitokeza na mtu unafikia hatua ya kuahirisha kufanya kile ambacho ulipanga kufanya.

kuahirisha

Sababu zinaweza kuwa kwamba hujajiandaa vya kutosha, wakati siyo mzuri au una mambo mengine mengi yanayokusubiri.

Lakini ukichimba kwa ndani sababu za nje zimekuwa siyo sababu za kweli za ndani. Sababu za nje zimekuwa ni sababu nzuri kuonekana kwa wengine, ambazo hawatakushangaa sana.

Lakini unapozama ndani, unakutana na sababu halisi, ambapo kubwa ni hofu. Hofu ya kushindwa, hofu ya kukataliwa na wakati mwingine hofu ya mafanikio inamfanya mtu ajione hajawa tayari kuchukua hatua.

Lakini unajiambiaje au unamwambiaje mtu kwamba hujaanza biashara kwa sababu unaogopa itashindwa? Si atakuona wewe ni mzembe? Lakini ukimwambia mtaji sina, hali ni ngumu, kila mtu anaelewa, si ndiyo?

SOMA; UKURASA WA 496; Nenda Kinyume…

Sasa leo nataka nikushirikishe fursa kubwa iliyopo kwenye tabia ya kuahirisha mambo. Japo wengi tunaiona kama kikwazo kikubwa kwa mafanikio yetu, inaweza pia kuwa kichocheo cha mafanikio yetu.

Jinsi ya kuitumia tabia hii kama kichocheo cha mafanikio ni kujisukuma kufanya kile unachotaka kuahirisha. Pale unapopanga kufanya kitu, halafu unapata sababu za kuahirisha, hapo hapo ndiyo unajipa ulazima wa kufanya.

Unapoanza kupata sababu za kuahirisha, jua hicho unachokwenda kufanya ni kikubwa na hivyo kazana kufanya. Hata kama huwezi kufanya kwa ukamilifu, angalau anza, na piga hatua ambayo baadaye itakuwa rahisi kuendelea. Usikubali kabisa kuahirisha kitu chochote ambacho umepanga kufanya na kinaweza kuleta matokeo makubwa kwako.

Fanya kile ambacho hupendi kufanya, kwa sababu vitu hivi mara nyingi ndiyo vyenye thamani kubwa kwetu na kwa mafanikio yetu. Unapopata ushawishi wa kuahirisha, hapo ndipo pa kuweka mkazo zaidi na kuhakikisha unafanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog