Habari za leo rafiki yangu?

Ni matumaini yangu kwamba upo vizuri na umeendelea kuwa na wakati bora sana kwako.

Kwa kipindi cha wiki moja iliyopita, tangu tarehe 21/12/2017 mpaka tarehe 27/12/2017 nilikuwa na likizo yangu ya wiki moja ya mwisho wa mwaka wa 2017. Huu ni utaratibu ambao nimekuwa nao kwa muda sasa wa kujipa muda wa kusoma kwa kina, kutafakari na kutahajudi na pia kuweka mikakati ya mwaka mzima.

Napenda kuchukua nafasi hii kukujulisha wewe rafiki yangu kwamba likizo yangu imeisha vyema na imekuwa likizo bora sana kwangu na kwako pia rafiki yangu.

Nimepata nafasi ya kujifunza baadhi ya vitu kwa kina, pia nimeweza kupitia kwa kina kila nilichofanya kwa mwaka 2017 na kuona ni namna gani kinachangia katika kufikia maono makubwa niliyonayo. Nimepata majibu makubwa na ya kunishangaza kidogo.

mafanikio 2018

Kwa kipindi hichi cha likizo, nilipanga kusoma vitabu saba, hivyo wastani wa kitabu kimoja kila siku, lakini nimesoma vitabu vinne pekee kati ya vitabu saba nilivyopanga kusoma.

Kilichosababisha nisome vitabu pungufu ya nilivyopanga ni utambuzi mkubwa nilioupata wakati nasoma baadhi ya vitabu. Vitabu karibu vyote nilivyopanga kusoma nilishavisoma tena siku za nyuma, hivyo nilipanga kurudia kuvisoma kwa kina zaidi na kuchagua vitu nitakavyofanyia kazi moja kwa moja kutoka kwenye kila kitabu.

Nilipata utambuzi mkubwa mno kwenye vitabu hivi ambao sikuwa nimeupata wakati navisoma kwa mara ya kwanza. Kuna vitu vilikuwa wazi kabisa kwenye kurasa za vitabu hivi lakini sikuviona wakati nasoma kwa mara ya kwanza. Na ninaposema kuwa wazi namaanisha ni dhana nzuri ambazo ningeweza kuzifanyia kazi lakini sikuzipata vizuri wakati nasoma kwa mara ya kwanza.

Hili limenifungua sana na kugundua huenda wakati nasoma kwa mara ya kwanza nilikuwa na kasi kiasi au sikuwa nimetulia vya kutosha kuweza kubeba kila ninachokutana nacho. Baada ya kusoma vitabu viwili ndani ya siku mbili za kwanza, nilijikuta nimeondoka na vitu vingi ninavyoweza kufanyia kazi mwaka mzima kiasi kwamba nikiendelea kusoma vitabu vingine vyote vilivyobaki labda sitavifanyia kazi kama nilivyotaka, au nitakutana na vitu vingi zaidi na hatimaye kushindwa kuchagua kipi hasa nianze nacho.

Hivyo nilimalizia kwa vitabu vingine viwili, ambavyo vilikuwa vinafanana kwa maudhui, na kwenye moja ya vitabu hivyo viwili nilivyomalizia kusoma, nikakutana na dhana nyingine kubwa sana ambayo itatuwezesha wote kupiga hatua kubwa kwenye biashara zozote tunazofanya.

Hivyo nilitumia muda mwingi kutafakari haya niliyojifunza kwa kina na kuchagua mambo makuu ambayo nitakwenda kuyafanya mwaka 2018 kuboresha maisha yangu na huduma zangu pia. Na nina hakika mambo haya yatakwenda kuyafanya maisha yako kuwa bora sana rafiki yangu.

Pia nilipata muda wa kutafakari na kutahajudi kwa kina, niliweza kupitia kila nilichoweza kufanya kwa mwaka 2017. Na nilipata mshangao mkubwa kwa sababu mwaka 2017 ni moja ya miaka ambayo nimejaribu kufanya vitu vingi na tofauti. Japo vingi vilikuwa vizuri kwa wengi, vilikuwa vinakwenda nje ya huduma zangu kuu ambazo napenda zaidi kuzitoa.

Hivyo mwaka 2018 nitakwenda kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye huduma ninazotoa. Ninakwenda kukusanya nguvu zangu na kuziweka kwenye maeneo machache ambayo yatakuwa na manufaa makubwa kwangu na kwako rafiki yangu, kuliko kutawanya nguvu zangu kwenye maeneo mengi ambayo yanaweza kuonekana mazuri lakini yasiwe na manufaa makubwa.

Hivyo basi kuna baadhi ya mambo nilikuwa nafanya nitaacha kabisa kuyafanya na mengine nitayapunguza kwa kiasi kikubwa sana. Nitaweka nguvu zangu kubwa kwenye njia yangu kuu ya kutoa mafunzo ambayo ni uandishi. Pia nilikuwa nikiandika kwenye maeneo mengi sana, hivyo nguvu zangu kusambaa mno. Ilikuwa vizuri na ujumbe unawafikia wengi, lakini kwa mwaka 2018 nitaweka nguvu zangu za uandishi kwenye AMKA MTANZANIA, KISIMA CHA MAARIFA na EMAIL ambazo nimekuwa natuma kwa wasomaji wa makala zangu.

Nimefanya upembuzi wa kina wa mitandao ya kijamii, japo nimeweza kupunguza sana muda ninaotumia kwenye mitandao hii, baada ya tafakari ya kina, nimegundua ni moja ya sehemu za kelele na usumbufu, ambazo nimekuwa natawanya nguvu zangu. Hivyo mwaka 2018 ni mwaka ambao sitatumia kabisa mitandao ya kijamii moja kwa moja, badala yake itabaki kama sehemu ya kazi zangu kusambaa zenyewe. Hapa namaanisha kwamba ninapoweka makala kwenye blog, basi inasambazwa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii. Lakini sitakuwepo moja kwa moja kwenye kila mtandao, kujibu maoni ya watu na kadhalika.

Katika tafakari ya kina niliyoifanya kwenye mitandao ya kijamii, nimegundua ninawafikia watu wengi, zaidi ya watu elfu 20, lakini wale wote ambao wamekuwa wanachukua hatua mbalimbali kwa mafundisho ninayoyatoa, wengi wanatoka kwenye email list, wale ambao wanapokea email ninazotuma. Hivyo email ninazotuma zina nguvu kubwa kuliko mitandao ya kijamii, kwa aina ya ujumbe ninaotoa na hatua ambazo napenda watu wachukue. Hivyo kama nitaweka nguvu kubwa kwenye emails, kwa kuongeza idadi ya emails ninazotuma na maarifa ninayotoa, nina imani wengi watapata manufaa makubwa zaidi.

Hivyo ambacho nitakuomba kwako rafiki yangu, ni kunisaidia kukuza email list yetu zaidi, kwa kuwaalika marafiki zako ambao unajua hawajawahi kusikia kuhusu mimi, uwaalike wajiunge na email list ili wawe wanapokea mafunzo haya moja kwa moja kwenye email zao. Unaweza kuwaalika kujiunga kwa kuwatumia link hii na wajaze fomu kujiunga. Link; https://landing.mailerlite.com/webforms/landing/u7i8s7

Maeneo mengine makubwa tunayokwenda kufanyia kazi mwaka 2018 ni mafunzo ya semina za mtandao na semina yetu ya moja kwa moja ya mwaka ya KISIMA CHA MAARIFA, ni maeneo ambayo nitapenda watu waondoke na thamani zaidi. Pia vitabu vitakuwa vingi zaidi kwa mwaka 2018, lakini huenda vyote vikawa kwa mfumo wa softcopy yaani PDF na vikawa vya kutuma kwa email. Hii ni baada ya kutafakari kwa kina mchakato wa kuchapa vitabu na kusambaza, unatawanya nguvu zangu zaidi. Hivyo kwa wale ambao hawawezi kusoma vitabu vya softcopy kwa kipindi hichi mtanisamehe kidogo.

Ukiangalia kwa kina tuna vitu viwili vikuu ambavyo ndiyo tunategemea sana kwenye maisha yetu, NGUVU NA MUDA. Tumekuwa tunakazana zaidi na muda, na pia nimeandika sana kuhusu muda, lakini tunasahau sana kuhusu NGUVU. Hivyo mtu unaweza kukazana ukapangilia vizuri muda wako, ukawa hupotezi muda kabisa, lakini bado ukawa hupigi hatua kubwa ambazo ulitegemea kupiga. Hivyo kusimamia vizuri nguvu zako na kuhakikisha zinakwenda sehemu sahihi na yenye matokeo bora kabisa ni hitaji muhimu sana la mafanikio yetu.

MASAA MAWILI YA ZIADA

Hivyo nitakushauri sana rafiki yangu, unavyoendelea kupangilia na kusimamia muda wako, angalia pia unasimamia na kupangiliaje nguvu zako. Kwa sababu hilo ni muhimu sana kama unataka kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Hakuna mtu anayeweza kufanya kila kitu, lakini kila mtu anaweza kufanya baadhi ya vitu kwa ubora wa hali ya juu sana. Je ni vitu gani ambavyo wewe unaweza kufanya kwa ubora wa hali ya juu sana? Vijue na kisha weka nguvu zako kwenye vitu hivyo na usikubali usumbufu wa aina yoyote ile ukuondoe kwenye vitu hivyo.

Nikuache na tafakari hiyo rafiki yangu, angalia maono makubwa uliyonayo, na kama bado huna basi semina inayokuja mwanzoni mwa mwaka 2018 itakusaidia kwenye hilo. Kisha angalia kila unachofanya kinakusaidiaje kufikia maono hayo makubwa, kama kuna vitu unafanya na havina msaada wa moja kwa moja, basi vinakuzuia wewe kufikia maono yako. Ni wakati sasa wa kuchagua kwa kina kipi ufanye na kipi usifanye ili uweze kufikia maono makubwa uliyonayo.

Nitaendelea kukushirikisha mengi zaidi niliyotoka nayo kwenye likizo yangu, na pia nitaendelea kukupa taarifa za semina yetu ya mwanzo wa mwaka 2018 pamoja na huduma nyingine ninazotoa.

Karibu sana tuendelee kuwa pamoja rafiki yangu, karibu sana tuendelee kuyafanya maisha yetu kuwa bora na kupiga hatua kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog