Kitu kimoja ambacho watu huwa hawaelewi haraka kwenye maisha ni kwamba, kila mtu anayatengeneza mazingira ya maisha yake, na kuna vitu ambavyo mtu anachagua kuvikuza kwa kujua au kutokujua.
Ukweli ni kwamba kwenye dunia tunayoishi ni vigumu sana kuujua ukweli. Kila mtu anaiangalia dunia kupitia miwani yenye rangi fulani. Rangi ya dunia unayoiona wewe siyo wanayoona wengine, kwa sababu inategemea umevaa miwani ya rangi gani.

Kile unachoona kwenye maisha yako, ndiyo kinachokua zaidi. Kile unachofikiri kwa muda mrefu ndiyo kinachotokea kwenye maisha yako. Unapata kile unachotafuta. Na wengi wasichojua, unachopambana nacho, ndiyo kinakua zaidi.
Unaweza kujiambia kwamba hupendi vitu fulani, lakini wewe kutokuvipenda siyo kwamba ndiyo umevifuta au kuviondoa, badala yake unaendelea kuvijenga zaidi kwenye maisha yako. Vile unavyopambana navyo, vile unavyovipinga na usivyovipenda ndiyo unavikuza zaidi kwenye maisha yako.
SOMA; UKURASA WA 598; Usichopenda Na Usichotaka….
Hivyo swali muhimu sana kwako ni je unachagua kukuza nini kwenye maisha yako?
Swali hili usijiulize tu kwa yale ambayo unataka yatokee kwenye maisha yako, badala yake jiulize kwenye kila unachojihusisha nacho. Kwa mfano, kama kuna kitu unahofia kwenye maisha yako, unakuwa umechagua kukikuza zaidi, hofu haiondoi kitu, bali inakikuza.
Kadhalika kwenye mahusiano yetu na wengine, unapobishana na mtu au kupambana naye, ndivyo unavyozidi kukuza nguvu zake za kupambana na kubishana na wewe. Hapo unakuwa umechagua kukuza ubishi na mapambano yake.
Hivyo rafiki, kuwa makini sana na kila kitu unachoruhusu kiingie kwenye akili yako au matendo yako. Iwe umedhamiria au hukudhamiria, unakuwa umetoa nafasi kwa kitu hicho kukua zaidi kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog