Ni siku mpya, siku nzuri, siku ya kipekee sana kwetu ambapo tuna nafasi nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii.
NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ndiyo msingi wetu mkuu wa mafanikio, ambao unatuwezesha kufanya makubwa.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ndiyo mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio kwa mwaka huu 2018.

Asubuhi ya leo tutafakari; FAIDA YA KUANZIA CHINI…
Kila mtu anapenda kuwa juu,
Kila mtu anapenda kuwa na mafanikio makubwa,
Kila mtu anapenda kuwa tajiri.
Lakini siyo wote wanaopata nafasi hizo za kuwa juu wananufaika nazo au hata kuweza kuzitunza.

Wapo wengi wanapata nafasi za kupanda juu haraka, lakini kinachofuata ni kuanguka, tena kuanguk vibaya.
Mifano ipo mingi ya watu waliorithi mali nyingi na wakapoteza zote,
Walioshinda bahati nasibu na kujikuta maisha yao yanakuwa hovyo zaidi.
Na wapo pia waliolipwa mafao au fidia kubwa, lakini baada ya muda wasijue malipo waliyopata yalipotelea wapi.
Hapo bado wale wanaoomba mkopo kwa matumizi fulani, lakini unaisha bila ya kufanya kile walichokuwa wanapanga kufanya.

Kuanzia chini, na hasa kukaa chini kwa muda na kujitengenezea njia ya kwenda juu, kuna faida nyingi kuliko kujikut ghafla uko juu.
Baadhi ya faida hizo ni kama;
đź’ĄHuna pa kwenda zaidi ya chini. Unapokuwa chini, huna pa kuanguka zaidi ya pale ulipo, hivyo unaweza kujaribu chochote bila ya kuwa na hofu ya kushindwa au kupoteza. Utapoteza nini kama huna chochote? Kuwa chini kunakupa uhuru ambao wengi waliopo juu hawawezi kuwa nao.

đź’ĄUnajifunza thamani ya juu na kuepuka kuanguka chini tena. Unapofanikiwa kutoka chini na kwenda juu, unajifunza thamani halisi ya kuwajuu na utaepuka kurudi chini tena.
Fedha ni fedha, lakini fedha uliyokota utaitumia hovyo kuliko fedha uliyoifanyia kazi kwa mateso.

đź’ĄHata ukianguka, utaweza kupanda tena. Wapo watu walioanzia chini, wakapambana na kufika juu, wakajikuta wameanguka tena chini. Lakini kwa sababu tayari wana uzoefu wa kutoka chini na kwenda juu, wanaweza kupanda tena juu.
Shida ipo kwa wale waiojikuta juu ghafla, wasijue wamefikaje pale, wakianguka ndiyo imetoka, hawawezi kurudi tena juu, maana hawajawai kufanya kitu kama hicho.

Kuna manufaa makubwa ya kuwa chini, usiogope unapokuwa chini na wala usiwadharau waliopo chini.
Kuna funzo kubwa sana kwenye safari ya kutoka chini kwenda juu, usikazane kutafuta njia za kukufikisha juu haraka na bila ya wewe mwenyewe kujua umefikaje juu.

Anzia chini na panda kwenda juu wewe mwenyewe, kadir unavyoweza. Jua thamani ya chini na jua thamanibya safari ya kutoka chini kwenda juu. Huenda kuna siku itarudia zoezi hilo.

Siku yako iwe bora sana rafiki yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha