Know, first, who you are, and then adorn yourself accordingly. – Epictetus
Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa nafasi hii nzuri sana ya leo.
Ni fursa ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Ni kwa msingi NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa sana leo.
Kwa mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo mwaka huu 2018 utakwenda kuwa wa kipekee sana.
Asubuhi ya leo tutafakari JIJUE KISHA JITUMIE…
Fikiria mtu ambaye ametumia fedha nyingi kununua kompyuta, halafu kazi pekee anayofanya kwenye kompyuta hiyo ni kusikiliza muziki.
Au mtu amenunua simu, lakini kitu pekee anachofanya na simu hiyo ni kuwasha tochi, kwa sababu simu hiyo ina tochi pia.
Hakika utashangaa, kwa nini mtu awe na kitu chenye uwezo mkubwa kiasi hicho, lakini anakitumia kwa kazi ndogo, ambayo ingeweza kufanywa na kifaa kingine kidogo na kinachopatikana kwa urahisi!
Lakini unapokuja kuangalia ukweli wa mambo, utagundua hichi ndiyo kila mmoja wetu anafanya.
Tuna uwezo mkubwa sana ndani yetu, lakini hatuutumii kabisa, tumeuacha tu umelala.
Tunatumia sehemu ndogo mno ya uwezo mkubwa ambao tunao kiakili na hata kimwili.
Akili zetu zinaweza kufanya zaidi ya tunavyofanya sasa.
Miili yetu inaweza kufanya zaidi ya tunavyofanya sasa.
Lakini wengi hawajui hilo, kwa sababu hawajaijua vizuri miili yao na akili zao.
Hawajajua kwa hakika uwezo mkubwa uliopo ndani yao.
Ndiyo maana leo nataka utafakari hili kwa kina.
Uweze kujua uwezo uliopo ndani yako, kisha uweze kuutumia.
Na katika kujua uwezo huo, usijionee huruma, badala yake jisukume mpaka tone la mwisho, pale unapoona ni mwisho wako, jisukume kwenda zaidi.
Njia pekee ya kujua ni mbali kiasi gani unaweza kwenda, ni kwenda mbali zaidi.
Anza sasa kwenda mbali kimwili na kiakili, na utaona namna ulikuwa unajinyima mengi kwa kutokwenda mbali.
Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha