Mahusiano yana nguvu kubwa sana kwenye maisha yetu ya kila siku. Tunasukumwa kuchukua hatua pale ambapo mtu ambaye tuna mahusiano naye ana uhitaji au matatizo yanayohitaji msaada wetu.

Katika mahusiano, kuna yale ya moja kwa moja, kama ya undugu, ambayo mtu hachagui. Kama mmezaliwa pamoja tayari mna uhusiano, na hivyo huchagui nani awe kaka yako au dada yako.

Lakini pia kuna yale mahusiano tunayotengeneza sisi wenyewe, haya ni mahusiano ya sisi wenyewe kupenda. Mahusiano haya ni kama ya urafiki na hata mahusiano ya kimapenzi.

Taaluma

Sasa haya mahusiano ya kuchagua sisi wenyewe, huwa ni mahusiano imara zaidi, kwa sababu hatulazimiki kuwa na mahusiano na watu tusiopenda kuwa na mahusiano nao.

Ninachosema ni kwamba, huwezi kuwakataa ndugu zako, na hata kama mtapishana au mkawa hamuendani kimtazamo, bado mtalazimika kuendelea kuwa ndugu.

Lakini kwa upande wa mahusiano ya kirafiki, unachagua mwenyewe na kama mtu hamuendani au mitazamo inapishana, hulazimiki kuwa na urafiki naye.

Sasa hii ndiyo nguvu kubwa sana unayopaswa kuitumia kwenye biashara yako, nguvu ya mahusiano ya kuchagua, mahusiano ya urafiki.

SOMA; BIASHARA LEO; Maswali Matatu Muhimu Kujiuliza Kuhusu Wateja Wa Biashara Yako.

Unapaswa kuwafanya wateja wa biashara yako kuwa marafiki zako, kwa wao wenyewe kukuchagua wewe uwe rafiki yao.

Na unafanya hivyo siyo kwa kuwaomba urafiki, bali kwa kuwajali, kuweka mahitaji na shida zao mbele kuliko maslahi yako binafsi.

Jiulize ni kipi kinakuvutia kwa marafiki ulionao, kisha kitengeneze hicho kwa wateja wako pia.

Kwa sehemu kubwa, jali mahitaji ya wateja wao, tatua changamoto zao na wasaidie pale wanapokwama kwenye eneo linalohusiana na biashara yako.

Pia hakikisha unakuwa mshauri wao mkuu kwenye eneo linalohusiana na biashara yako. Kwa njia hii wataona thamani unayoongeza kwao na watakujali sana.

Muhimu, urafiki haimaanishi wewe uingie hasara kwa sababu ya wateja wako, wala haimaanishi uwakopeshe wateja wako, au kufanya chochote ambacho kinaumiza biashara yako. Tofautisha kabisa hayo kwenye urafiki wako na wateja wako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog