Akili zetu sisi binadamu ni kitu cha ajabu sana, ni kitu ambacho kina nguvu ya kufanya makubwa kuliko tunavyoweza kutegemea. Lakini cha kushangaza ni kwamba, mtu anaweza kuitawala akili yake akafanya makubwa, au akatawaliwa na akili yake na kuwa mtumwa maisha yake yote.

Tumekuwa tunaona watu wengi wakiingia kwenye uraibu (addiction) wa madawa ya kulevya, pombe na hata sigara. Lakini siku za hivi karibuni, umekuja uraibu mpya ambao ni matumizi ya mitandao ya kijamii, ni kitu ambacho kwa kuangalia kwa haraka ni kizuri na hakina madhara, lakini kwa ndani, kimekuwa sumu kubwa.

Watu wamekuwa wanajijengea tabia, ambazo baadaye zinakuwa uraibu na ngumu sana kuvunja.

Mwandishi Judson Brewer kwenye kitabu chake cha THE CRAVING MIND anatuonesha jinsi ambavyo tunatengeneza tabia, kisha tabia hizi zinakuwa uraibu kwetu. Pia amejadili kwa kina sana uraibu wa sigara, uraibu wa mitandao ya kijamii, uraibu wa mawazo binafsi na hata uraibu wa mapenzi. Mwandishi anatuonesha namna ambavyo tunajitengenezea magereza yetu wenyewe na njia sahihi ya kuvunja magereza haya na kuwa huru tena.

craving mind

Karibu tujifunze kwa pamoja kuhusu uraibu na jinsi ya kuvunja tabia mbaya kupitia kitabu hichi cha THE CRAVING MIND.

JINSI TUNAVYOTENGENEZA URAIBU NA TABIA MBAYA.

 1. Maana ya uraibu/uteja.

Uraibu ni ile hali ya kuendelea kufanya kitu, au kutumia kitu licha ya kitu hicho kuwa na madhara kwa mtu. Mtu anakuwa anaumia kwa kufanya au kutumia kitu, lakini pia hawezi kuacha kukitumia. Hapa ndipo mtu anakuwa amejenga gereza ambalo analijutia, ila pia hawezi kuondoka. Tumekuwa tunaliona hili kwenye madawa ya kulevya, pale mtu anapokuwa amedhuriwa sana na madawa hayo, ila pia hawezi kuyaacha, maana kuyaacha kunafanya ajisikie vibaya zaidi. Unataka kujua uraibu mpya na kwa wengi sasa? Matumizi ya mitandao ya kijamii, utawasikia watu wakisema mitandao inawapotezea muda, lakini bado wanaendelea kuitembelea kila mara, wakikaa muda kidogo bila kuifungua wanaona kama kuna kitu kikubwa wanakosa.

 1. Hatutofautiani na wanyama wadogo kwenye kujenga tabia.

Binadamu sisi ni viumbe ambao tuna uwezo mkubwa wa kufikiri na kufanya maamuzi ukilinganisha na wanyama na viumbe wengine hai. Lakini linapokuja swala la kujenga tabia, hatutofautiani kabisa na wanyama wadogo kama minyoo. Msingi mkuu wa kufanya maamuzi kwa viumbe wote hai unasukumwa kuchukua hatua ili kuendelea kuwa hai. Na hatua hizi ni kuelekea kulipo na chakula na kuondoka kwenye hatari.

Huwa tunafanya maamuzi kwa kusukumwa na vitu viwili, kupata tunachotaka au kuepuka kukosa au hatari. Hivi pia ndivyo tunavyojenga tabia, tunaanza kufanya kile ambacho kinatuna tunachotaka na baadaye inakuwa tabia. Au kuepuka ambacho ni hatari na kisha kuwa tabia.

 1. Hatua tatu za kutengeneza tabia yoyote.

Katika kujenga tabia, zipo hatua tatu ambazo huwa tunazipitia, hatua hizi zinafanya tabia iwe imara kwetu na iwe vigumu kuvunja.

Hatua ya kwanza ni kichocheo, hapa kunakuwa na kitu ambacho kinachochea mtu kuchukua hatua. Kwa mfano kwa mtu ambaye ameshajijengea tabia ya kuvuta sigara, inaweza kuwa kujisikia vibaya kukawa kichocheo chake cha kuvuta sigara.

Hatua ya pili ni tukio, baada ya kupata kichocheo kinachofuata ni tukio la tabia husika. Tukio ndiyo linakamilisha tabia husika.

Hatua ya tatu ni zawadi. Hichi ni kile ambacho mtu anapata baada ya kutekeleza tukio fulani. Hapa mtu anapata zawadi fulani ambayo inamfanya aone hatua aliyochukua ni muhimu. Kwa mfano kwenye uvutaji sigara, mtu anajisikia vibaya, anavuta sigara, halafu zawadi inakuwa kujisikia vizuri.

Kitu kikubwa kinachofanya tabia iwe sugu ni KURUDIA. Ili mtu apate tena ile zawadi aliyopata, anarudia tena huo mzunguko wa KICHOCHEO-TENDO-ZAWADI. Na hapo ndipo mtu anaweza kuvuta sigara zaidi ya kumi kwa siku, au kutembelea mitandao ya kijamii kila mara, ili kupata ile zawadi.

 1. Kufanya bila ya kufikiria (mindless).

Baada ya kuwa tumeshajitengenezea tabia, kinachofuata ni mtu kuchukua hatua bila hata ya kufikiria. Yaani kinachotokea unakuta mtu anafanya kitu, lakini hajui kama hata amefanya, hapa tabia inakuwa imeshaingia ndani ya mtu. Na hapa pia ndipo inapokuwa vigumu kuvunja tabia, kwa sababu sasa tabia haipo tena chini ya maamuzi ya mtu. Mtu anajikuta ameshachukua hatua, kwa mfano, ukigusa moto, moja kwa moja utaondoka haraka kwenye moto huo, wala hutafikiria mara mbili.

Hivyo kichocheo kinapotokea, tabia inafanyika bila hata ya mtu kujua. Hili pia ndiyo eneo zuri la kuvunja tabia kwa sababu mtu ukianza kufikiria kwa kina kila unachofanya, unaanza kuona vichocheo vya tabia na kuweza kuchukua hatua mbadala.

UBONGO KWENYE UTENGENEZAJI WA TABIA.

Ubongo wetu unahusika sana kwenye utengenezaji wa tabia, kuanzia kichocheo, hatua za kuchukua mpaka zawadi ambayo mtu unapata kwa hatua unayochukua.

 1. Mgawanyiko wa ubongo katika kufanya maamuzi.

Upo ubongo wa chini ambao unafanya maamuzi bila ya kufikiri na upo ubongo wa juu ambao unafanya maamuzi kwa kufikiri. Inapokuja kwenye tabia, mwanzoni mwa tabia, ubongo unaofikiri ndiyo unaofanya maamuzi ya kuchukua hatua, lakini kitu kikishakuwa tabia, kikishakuwa uraibu, ubongo unaofanya maamuzi unakosa nguvu na ubongo wa chini usiofanya maamuzi ndiyo unatawala. Ndiyo maana mtu anaweza kufanya jambo la hovyo kabisa ili kukamilisha tabia fulani, mfano mteja wa madawa ya kulevya anaweza kuuza kitu cha thamani kubwa kwa bei ndogo ili tu apate madawa ya kulevya.

 1. Kemikali ya Dopamine ndiyo inahusika na ujengaji wa tabia.

Katika hatua tatu za kutengeneza tabia, hatua ya tatu ambayo ni zawadi, kinachofanyika ni kemikali ya dopamine kuachiliwa kwenye ubongo na mtu kujisikia vizuri. Kemikali hii ndiyo inawafanya watu kujisikia vizuri na ili kuipata tena wanahitaji kurudia tena tabia hiyo.

Changamoto ni kwamba kemikali hii hudumu muda mfupi, hivyo ili mtu apate tena kujisikia vizuri, anahitaji kurudia tena tabia hiyo. Ni kwenye kurudia huku ndipo uraibu huzaliwa na kumfanya mtu kuwa mteja wa kitu fulani.

 1. Msongo wa mawazo unazima ubongo wa juu unaofanya maamuzi.

Changamoto kubwa kwenye kuvunja tabia yoyote ile ni msongo wa mawazo. Mtu anaweza kupanga kuondokana na tabia fulani ambayo siyo nzuri kwake, mambo yakiwa vizuri, anaweza kweli kuacha, lakini kinapotokea kitu ambacho kinamfanya awe na msongo wa mawazo, mtu hujikuta anarudi kwenye tabia anayotaka kuacha.

Hii ni kwa sababu msongo wa mawazo huzima ubongo wa juu ambao ndiyo unahusika kufanya maamuzi. Unapokuwa na msongo wa mawazo, akili yako inachukua kwamba upo kwenye hali ya hatari, hivyo unajikuta unachukua hatua bila hata ya kufikiri. Hii ndiyo inawarudisha wengi kwenye tabia wanazotaka kuacha. Kwa mfano mtu anataka kuondokana na ulevi, ghafla akapata taarifa mbaya za msiba, akawa na msongo na kujikuta anatumia pombe ili kuondokana na msongo huo.

MATUMIZI YA AKILI KATIKA KUVUNJA TABIA MBAYA.

Kwa kuwa tumeona ujengaji wa tabia unaanzia kwenye akili zetu, hivyo hata kuzivunja lazima kuanzie kwenye akili zetu pia. Tumeona tabia nyingi zinatokea bila hata ya sisi kufikiria (mindlessness) hivyo kama tukianza kufikiri kwa kina kwa kila tunalofanya (mindfulness) tutaweza kuona kichocheo cha tabia na kuamua kuchukua hatua tofauti.

 1. Kutumia uwepo kwenye kuvunja tabia.

Mara nyingi huwa tunafanya mambo huku akili zetu zikiwa hazipo kabisa (mindless), hivyo kama tutaanza kutumia uwepo wa akili zetu (mindful) tutaweza kuvunja tabia nyingi mbaya.

Kutumia uwepo ni kuona kile ambacho kinatokea pale ulipo, kama ambavyo kinatokea, kisha kuchukua hatua sahihi ili kupata matokeo bora. kutumia uwepo siyo kujihukumu au kujizuia usifanye tabia fulani, bali kuangalia kwa kina kipi kinakupelekea kufanya tabia hiyo. Kwa mfano kama kila unapogombana au kupishana na mtu unakimbilia kwenye mitandao ya kijamii, angalia hilo pale unapogombana na mtu, na pale unapotaka kukimbilia kwenye mitandao ya kijamii, kaa kwanza na hitaji hilo, lakini usilitekeleze.

 1. Hatua nne za kutumia uwepo kiakili kuvunja tabia.

Hatua ya kwanza; tambua lile hitaji la kutekeleza tabia fulani, jua kichocheo cha tabia.

Hatua ya pili; kubali kichocheo hicho kiwepo, usikazane na kichocheo, huwezi kukibadili.

Hatua ya tatu; kichunguze kichocheo hicho kwa kina, angalia jinsi mwili wako unakusukuma kuchukua hatua, hapa jifunze lakini usichukue hatua yoyote.

Hatua ya nne; fuata kichocheo hicho mpaka kinapoondoka. Usikubali kuchukua ile hatua unayochochewa kuchukua, badala yake fuatilia kichocheo hicho mpaka kinapoondoka, bila ya kusalimu amri kwa kichocheo hicho.

Kwa hatua hizi nne, unavunja ile hali ya kuchukua hatua bila ya kufikiri na kujikuta ukijilaumu kwamba kwa nini umefanya.

 1. Ukivunja tamaa, unaweza kuondokana na tabia mbaya.

Kinachowafanya watu wengi kuendelea na tabia mbaya ni kushindwa kuzia tamaa zao, hasa pale zinapokuja kwa nguvu kubwa. Kusalimu amri kwa tamaa zako ndiyo kitu kinachofanya tabia mbaya kuendelea kuwepo. Ukivunja tamaa ambazo unazo, na siyo kwa kutumia nguvu, bali kuiona tamaa lakini kutokuchukua hatua yoyote unavunja zile hatua za kujenga na kuendeleza tabia.

URAIBU WA MITANDAO YA KIJAMII.

Mitandao ya kijamii imekuwa aina mpya ya uraibu kwa wengi. Wengi wamejikuta wanakuwa watumwa wa mitandao hii, wakiitumia kwa muda mrefu huku wakitaka kuacha lakini wasiweze. Mitandao miwili, facebook na instagram ndiyo imekuwa na uraibu mkubwa kwa wengi.

 1. Mitandao ya kijamii imetengenezwa kutengeneza utegemezi.

Kwa namna mitandao hii ilivyotengenezwa, ni makusudi kwa ajili ya kukufanya uitembelee mara kwa mara. Kwa mfano unapoandika kitu, au unapoweka picha, kuna vitufe vya kupenda na eneo la kuweka maono. Hivyo ukishaweka ujumbe wako au picha yako, kila wakati utahitaji kuangalia je ni watu wangapi wamependa ujumbe au picha hiyo (umepata like ngapi) na pia kuangalia je watu wanasemaje kwenye maoni? Je wanakusifia? Je wapo walioweka maono mabaya? Hivyo hili linakulazimu kila mara uangalie nini kinaendelea.

Hivi umewahi kujiuliza kwa nini mitandao ya kijamii ina kitufe cha kupenda (like) lakini haina kitufe cha kutokupenda (dislike)? Kwa sababu inakuvutia uangalie likes ngapi umepata.

 1. Mitandao ya kijamii na dopamine.

Unapoingia facebook au instagram, ukaweka ujumbe au picha yako, ukaona marafiki zako wanakupa likes, na wengine wanasema uko vizuri, umependeza, mara moja dopamine inaachiliwa kwenye ubongo wako na unajisikia vizuri. Unapotoka kwa ajili ya kufanya mambo mengine, ukiwa unajisikia vibaya, utajiambia uchungulie tena kwenye mtandao kuona nini kimeendelea. Ukiona ujumbe umekuja kwamba una likes 20 na maoni 5, haraka haraka unataka kujua nani kalike na nani kaacha ujumbe na ujumbe gani. Hivyo kwa haraka unakimbilia kufungua, na kadiri unavyoona watu wana like, ndivyo dopamine zaidi inaachiliwa na kujisikia vizuri. Hii sasa inakuwa tabia, kila ukijisikia vibaya unaingia kwenye mtandao kupata dopamine kidogo. Na hivi ndivyo uraibu wa mitandao ya kijamii unavyotengenezwa.

 1. Uraibu wa mitandao ya kijamii ni chanzo cha sonona.

Tafiti zinaonesha kwamba, uraibu wa mitandao ya kijamii kimekuwa chanzo kipya cha ugonjwa wa sonona (depression) kwa wengi. Kwa mfano mtu anapoweka picha au ujumbe wake, halafu watu wasiupende au wakaweka maoni mabaya, huku mwingine akiweka ujumbe au picha anapata likes nyingi au maoni mengi, inapelekea watu kuanza kujilinganisha na kuona wao hawajakamilika.

Wengine wanapoona wenzao wanaweka picha za kuonesha maisha yao ni mazuri, wakila vyakula vizuri, wakiwa maeneo ya starehe, wanaona wenzao wana maisha mazuri huku wao wakiwa na maisha mabaya, wasijue kwamba kila mtu anapenda kuweka picha za mambo mazuri, lakini yale mabaya hawaweki, na kila mtu ana mambo yake mabaya.

 1. Kuondokana na uraibu wa mitandao ya kijamii, tumia uwepo na angalia ukweli.

Unahitaji kutumia uwepo, hasa pale unapojisikia vibaya na kuona sehemu pekee ya kukimbilia ni mitandao ya kijamii. Usikubali kukimbilia mitandao hiyo, badala yake kaa na hali hiyo ya kujisikia vibaya na utajifunza hatua sahihi za kuchukua.

Pia tumia akili na acha kujilinganisha na maisha ya mitandaoni. Jua kabisa kile watu wanaweza kwenye mitandao, ni sehemu ndogo sana ya maisha yao. Mtu anaweza kula makande kila siku asiweke picha, akala kuku siku moja na kuweka picha kwenye mitandao, wewe ukaona kwamba huwa anakula kuku kila siku, kumbe siyo sahihi. Jua kila mtu ana matatizo na changamoto zake, na yale watu wanaweka kwenye mtandao, siyo maisha yao ya kila siku.

URAIBU KWENYE KELELE.

Tunaishi kwenye zama ambazo ni za kelele, kila mtu anapiga kelele na ubaya zaidi ni kwamba kelele hizi zipo na sisi masaa 24 ya siku, tunakuwa nazo kabla hatujalala na tukiamka ndiyo kitu cha kwanza tunaanza nacho. Haya yote yamewezeshwa na kifaa kidogo sana, ambacho tunaenda nacho kila mahali mpaka kitandani. Kifaa hicho ni simu janja au kama inavyojulikana kwa kiingereza ‘smartphone’. Simu janja zimekuwa chanzo kikuu cha kelele kwenye maisha yetu na wengi tumeshakuwa na uraibu na simu zetu.

 1. Jinsi ya kupima kama una uraibu wa simu yako, yaani umeshakuwa mteja kwa simu yako.

Katika maelezo hayuatayo, jipe alama moja kama ni kweli kwako.

Moja; natumia simu yangu kwa muda mwingi zaidi ya ninavyotegemea.

Mbili; napenda kupunguza muda ninaotumia kwenye simu lakini nashindwa.

Tatu; natumia muda mwingi kujaribu kuacha kutumia simu.

Nne; ninapata tamaa ya kutumia simu kila mara.

Tano; nashindwa kufanya kazi vizuri, kazi vizuri au hata kusoma vizuri kwa sababu ya simu.

Sita; matumizi yangu ya simu yameleta matatizo kwenye mahusiano yangu.

Saba; nimekuwa napitwa na mambo ya kijamii na hata kupumzika kwa sababu ya matumizi ya simu.

Nane; nashindwa kuacha kutumia simu licha ya kuniweka kwenye hatari (mfano kutumia huku unaendesha gari).

Tisa; unaendelea kutumia simu licha ya kwamba imekuletea matatizo mbalimbali kimwili au kisaikolojia.

Kumi; kuhitaji kutumia simu zaidi na zaidi kadiri siku zinavyokwenda.

Kumi na moja; huwezi kukaa mbali na simu yako hata kwa muda mfupi.

Jumlisha alama ulizopata kwenye maelezo yako, kama jumla ni 2-3 una uraibu kidogo, alama 4-5 una uraibu kiasi na alama 6-7 una uraibu uliozidi kiasi.

 1. Tangu matumizi ya simu janja yameanza, ajali za watoto zimekuwa nyingi.

Tafiti zilizofanywa nchini marekani zinaonesha kwamba tangu matumizi ya simu janja yameanza, ajali za watoto zimeongezeka mara dufu. Na ukilinganisha maeneo yenye matumizi makubwa ya simu janja na yenye matumizi madogo, maeneo yenye matumizi makubwa ndiyo yana ajali nyingi.

Hii yote inaonesha kwamba, matumizi ya simu janja yamepunguza umakini wa watu katika kulea watoto wadogo. Hasa pale mzazi au mlezi anapokuwa bize na simu halafu mtoto akamponyoka na kwenda kufanya kitu hatari kwake.

 1. Kuondokana na uraibu wa kelele na simu, tumia uwepo.

Mara nyingi tunakuwa wateja wa kelele na simu zetu kwa kutaka kukimbia hali tunazokuwa nazo au kutaka kujua nini kinaendelea, kuepuka kupitwa. Njia sahihi ya kuondokana na hili ni kutumia uwepo kiakili. Ambapo unakubali kutulia na hali uliyonayo na pia kujua hakuna unachokosa. Pia kuwa na subira, kwa mfano kupokea simu au kuandika ujumbe ukiwa unaendesha ni hatari, lakini watu wanafanya mara zote kwa sababu hawana subira.

URAIBU WA MAPENZI.

Mapenzi pia yamekuwa ni uraibu kwa wengi, hasa pale mapenzi yanapokuwa mapya na watu kuwafikiria zaidi wapenzi na hilo kuwafanya wasione uhalisia wa mambo. Hili huwapelekea watu kufanya maamuzi mabovu ambayo baadaye yanawagharimu.

 1. Upofu wa mapenzi ni uraibu.

Watu wengi wanapoanza mapenzi huwa hawasikii la kuambiwa wala hawaoni la kuona. Wanawaona wenza wao kama ndiyo watu walioletwa kwa ajili yao. Na hata wanapooneshwa mambo yaliyo wazi kabisa kuhusu wenza wao, husema ni wivu au watu hawajui.

Hii husababishwa na uraibu, ambao unatokana na mtu kumfikiria zaidi mwenza wake muda wote. Na kila anapomfikiria, ubongo unapata dopamine ambayo inamfanya ajisikie vizuri. Hivyo anajikuta akirudia hilo kila mara. Ni mpaka pale mambo yanapotokea ambayo yanamfanya mtu kuona tofauti ndipo anaona wazi kwamba alikuwa akijidanganya.

NJIA KUU YA KUONDOKANA NA URAIBU.

Tumeona tangu mwanzo kwamba uraibu unatokana na kukosa uwepo, ambapo mtu unajikuta unafanya kitu bila hata ya kufikiria. Na njia ya kuondokana na hali hii ni kuwa na uwepo kiakili kwa kila unachofanya.

 1. Tahajudi inakusaidia kuwa na uwepo na kuvunja uraibu.

Tahajudi inatupa njia rahisi ya kudhibiti mawazo yetu na kuepuka kuchukua hatua bila ya kufikiri. Kupitia tahajudi, unaweza kuifanya akili yako itulie kabla ya kukimbilia kuchukua hatua. Kwa kufanya tahajudi, mtu unaimarisha uwezo wako wa kuwa na uwepo kwenye kila unachofanya.

 1. Mafunzo ya Buddha; maisha ni mateso.

Tahajudi imetokana na mafunzo ya kifalsafa na kiimani ya Buddha. Ambapo msingi mkuu wa mafunzo haya ni maisha ni mateso. Na watu wamekuwa wanazidisha mateso hayo kwa kukazana kutimiza tamaa na matakwa yao, wakifikiri wanapunguza mateso.

Njia pekee ya kupunguza mateso ya maisha Buddha anasema ni kuvunja tamaa na kutoshikiza furaha ya maisha yako na kitu chochote. Ukiweza kufikia hatua hii hutasumbuliwa na uraibu wa kitu chochote kile. Kwa sababu unajua kila kitu kwenye maisha kinakuja na mateso yake, hivyo maisha yako yanapokamilika bila ya kitu, huwi mtumwa.

Hata ukiangalia walevi, walianza kunywa wakifikiri pombe itawaondokea mateso au mawazo, lakini pombe au madawa yamewaletea mateso zaidi. Kadhalika matumizi ya mitandao ya kijamii, wengi hufikiri ni njia ya kuondokana na hali ya kujisikia vibaya, lakini inazalisha matatizo zaidi.

Hayo ndiyo muhimu ya kukushirikisha kwenye kitabu hichi cha THE CRAVING MIND, ni kitabu kizuri sana ambazo kinaendana na changamoto tunazopitia kwenye zama tunazoishi sasa.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

Usomaji