Rafiki yangu mpendwa,

Ni kitu gani hasa unachokitaka kwenye maisha yako? Kinachokunyima usingizi, kinachokufanya ufikiri wakati wote? Ni kitu gani kinachokuamsha asubuhi na mapema na kukufanya uache kitanda?

Je ni fedha nyingi kiasi kwamba hutakuwa tena na wasiwasi pale unapokutana na changamoto zinazohitaji fedha? Au ni kujulikana na wengi kupitia kile unachofanya?

Kila binadamu aliye hai, anapenda kupata mafanikio zaidi. Anapenda kutoka pale alipo sasa na kwenda mbali zaidi. Anapenda kuwa na maisha bora zaidi ya aliyonayo sasa.

Lakini kutaka tu na kupenda haitoshi, maana asilimia kubwa ya watu wanapenda na kutaka vitu fulani, lakini wengi hawavipati.

Dunia ni kama inatutega, ina kila tunachotaka, lakini haitoi kwa urahisi. Ni sawa na kuwa na mtu ambaye ana chochote unachotaka, lakini hakupi kirahisi, kila ukimwambia unataka anakuambia bado hujawa tayari. Sasa usipojua jinsi ya kumtega mtu huyo akupe unachotaka, hutakipata na hutakuwa tayari.

MIMI NI MSHINDI

Ili dunia ikupe kile unachotaka, iwe ni fedha nyingi sana, umaarufu au mafanikio yoyote unayotaka, unahitaji kujua njia bora ya kuitega dunia. Unahitaji kuitega dunia kwa namna ambayo itakuwa tayari kukupa kile unachotaka kwa kuamini upo tayari kukipokea na kukitunza.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Craving Mind (Jinsi Tunavyonasa Kwenye Uraibu Na Jinsi Ya Kuvunja Tabia Mbaya.)

Kila unapoanza kufanyia kazi mipango yoyote kwenye maisha yako, kikubwa ambacho umekuwa unakutana nacho ni changamoto na vikwazo. Wengi huishia kukubali changamoto na vikwazo hivyo na kuona hawawezi kuendelea tena. Hii ni njia ya kwanza ya dunia kutupima, kutaka kujua je kweli tumejitoa kwa kile tunachotaka? Au tunajaribu jaribu tu. Maana dunia huwa haiwapendi watu wanaojaribu, inapenda watu wanaofanya, na wanaojitoa kweli ili kupata kile wanachotaka.

Njia bora ya kuitega dunia ikupe chochote kile unachotaka ni kuwa wa thamani sana, kutoa thamani kubwa sana kwa dunia. Unahitaji kutoa thamani kubwa sana ambayo haijawahi kuonekana duniani, na hapo dunia itajua kweli umejitoa kupata unachotaka. Na kupitia thamani hiyo unayotoa, dunia itaanza kukupa chochote unachotaka.

Kwa sababu umeipa dunia kitu ambacho hakijawahi kuonekana, dunia haitakubali kukuacha kirahisi, itataka uendelee kutoa thamani hiyo zaidi, hivyo itakupa kila unachotaka ili uendelee kutoa thamani hiyo kubwa.

Hii ni sheria kabisa na siyo kubahatisha, unapofanya kile cha thamani, kile ambacho hakijazoeleka na watu wanakihitaji kweli, watu watakuwa tayari kukupa kile unachotaka ili wapate hiyo thamani uliyozalisha.

Kazana sana kutoa thamani kubwa kwenye chochote kile unachoruhusu mikono yako ishike, usikubali kuwa mtu wa kawaida, anayefanya vitu vya kawaida ambavyo kila mtu anaweza kufanya. Dunia haiwajali watu wa aina hiyo, maana wapo wengi na hivyo hata wakipotea wachache bado dunia itaenda vizuri.

Lakini wale wanaofanya makubwa, wale ambao wanafanya ambayo hayajazoeleka na hakuna mwingine anayeweza kufanya, dunia inawaheshimu, dunia inawalinda na kuwapa chochote wanachotaka na kuhakikisha wanaendelea kutoa thamani hiyo wanayoitoa.

Chochote unachochagua kufanya na muda wako rafiki, kifanye kwa viwango vya hali ya juu sana. Hakikisha unafanya kwa viwango ambavyo havijazoeleka, viwango vya kipekee kabisa na vinavyofanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.

Nikupe angalizo rafiki yangu, pamoja na kwamba kwa kutoa thamani kubwa dunia itakupa chochote unachotaka, siyo mara zote utapata matokeo haraka kama unavyofikiri. Wakati mwingine itakuchukua muda, utahitaji kutoa na kutoa na kutoa kabla hujaanza kupokea. Wakati mwingine utaanza kutoa thamani na wengine wataiga na kujikuta unachofanya kila mtu anafanya. Hivyo unahitaji kuwa mvumilivu, unahitaji kuwa mtu wa kujituma mara zote na kupiga hatua zaidi kwa kila siku mpya unayoipata.

Nenda kafanye makubwa leo rafiki yangu, nenda katoe thamani kubwa sana, nenda kaipe dunia kitu ambacho haijawahi kupata na utakuwa kwenye nafasi kubwa ya kupata chochote unachotaka.

SOMA; Tumia Siri Hii Moja Kupata Chochote Unachotaka Kwenye Maisha Yako.

Nikushirikishe falsafa ambayo nimekuwa naishi nayo, falsafa ambayo nilijifunza kutoka kwa Zig Zigler, falsafa ambayo ninaiamini na najua itanipa kila ninachotaka. Zig Zigler alisema “unaweza kupata chochote unachotaka kupata, kama utawasaidia watu wengi zaidi kupata kile ambacho wanataka”. Hebu angalia kwenye lile eneo lako, kwenye kile ulichochagua kufanya, ni kitu gani hasa wengi wanataka? Kazana kuwapa wengi zaidi kitu hicho, na dunia haitakuacha salama, bali itakupa kila unachotaka kupata. Unapowapa watu hao kile wanachotaka haimaanishi unagawa vitu fulani bure, ina maana kwamba unatoa thamani kubwa ya kuwapa kile ambacho wanaihitaji sana na wapo tayari kukilipia ili kupata. Na pia kuna wakati unahitaji kutoa bila ya kulipwa chochote, lakini ukijua kwamba dunia haitakuacha bila ya kukulipa.

Ipe dunia kile unachotaka, toa thamani kubwa sana kwa dunia na utaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji