Rafiki yangu mpendwa,

Tuwe tu wakweli, huwa unajisikiaje pale unapokutana na mtu ambaye mlijuana siku za nyuma, mlikuwa sawa wote, lakini sasa amepiga hatua sana kuliko wewe?

Labda ni mtu mlisoma naye, na darasani wala hakuwa na uwezo mkubwa sana, lakini sasa hivi amepiga hatua sana kuliko wewe.

Au hata ni mdogo wako, ambaye hakuna na utofauti mkubwa tangu utoto wake, lakini sasa hivi huwezi kukaa pale anapokaa yeye.

Zipo hali nyingi kwenye maisha yetu ambazo zinaibua hisia za wivu ndani ya kila mmoja wetu. Pale tunapoona watu ambao tunawajua vizuri kwamba walikuwa wa kawaida ila wameweza kupiga hatua kubwa sana.

Wengi wanapopata hisia hizi za wivu, kwanza huanza kujiambia hawaoni wivu, ila sasa kinachotokea wanajenga chuki. Wanaanza kuwachukia wale watu waliopiga hatua kuliko wao, bila hata sababu ya msingi. Mtu anatamani ndani ya moyo wake mtu yule ashindwe au kuanguka ili ionekane kwamba hakuwa na uwezo wa kupata mafanikio kama hayo. Wewe unafikiri kwa nini watu waliofanikiwa wakikutana na changamoto kidogo basi jamii nzima huwa inafurahia na kila mtu kusema yake? Wivu!

Wengine hukabili hisia za wivu kwa kukataa, ndani yao wanakataa kwamba yule aliyepiga hatua kubwa kuliko wao hajaweza kupiga hatua hizo mwenyewe. Hapa ndipo watu husema kwamba mtu yule alipata bahati fulani, au alipendelewa au alikuwa na bahati. Yote haya hayana hata chembe ya ukweli kwenye mafanikio, kwa sababu kama ingekuwa ni bahati au kupendelewa pekee, wapo wengi wanaopata nafasi kama hizo lakini hawafanikiwi.

FEDHA KWA BLOG

Njia hizo mbili na nyingine nyingi ambazo watu wanazitumia kukabiliana na wivu unaoibuka ndani yao juu ya wengine, siyo njia sahihi kwa sababu hazikusaidii wewe unayepata hisia za wivu, zaidi ya kukujengea chuki na hata kukata tamaa.

Kwenye makala hii nakwenda kukushirikisha njia tano za kukabili hisia za wivu pale zinapoibuka kutokana na mafanikio ya wengine. Njia hizi zitakuwezesha wewe kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako kupitia hamasa ya wengine ambao wamepiga hatua.

Moja; acha kujilinganisha na wengine.

Maisha siyo mchezo wa kulinganishana, watu tunatofautiana na hakuna watu wawili wanaofanana kwa kila kitu hapa duniani. Hata mapacha wanaofanana kwa nje, ndani yao bado hawafanani.

Kila mmoja wetu ni wa kipekee, kila mtu ana uwezo mkubwa ndani yake wa kuweza kufanya vitu ambavyo hakuna mtu mwingine hapa duniani anaweza kufanya.

Hivyo unapomwona mtu amepiga hatua kubwa kwenye maisha yake, jua ameweza kutumia vizuri uwezo wako. Hivyo unachopaswa kufanya siyo kumwonea wivu, bali kujua yeye ni tofauti na yeye na kilichomfanya afanikiwe yeye siyo kitakachokufanya ufanikiwe wewe.

Kazana kujua upekee wako na uwezo mkubwa uliopo ndani yako na utumie ili kuweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Mbili; jua hakuna njia moja ya kuelekea kwenye mafanikio.

Kwa sababu mtu fulani unayemjua amefanikiwa kwenye uandishi, haimaanishi na wewe utafanikiwa kupitia uandishi. Kwa sababu mtu unayemjua amefanikiwa na kuwa msanii mkubwa, haimaanishi na wewe ukiingia kwenye usanii utafanikiwa.

Hakuna njia moja ya mafanikio ambayo ukishaingia kwenye njia hiyo lazima utafanikiwa. Ndiyo maana kwenye kila eneo la maisha, wapo watu waliofanikiwa sana na wapo watu walioshindwa kabisa. Hata kama utaambiwa fursa hii ni nzuri sana, imetengeneza matajiri wengi, wewe angalia kwa makini na utakuta masikini wengi pia kwenye fursa hiyo.

Hivyo unapomwona mtu mwingine amepiga hatua na kufanikiwa, wala usiwe na wivu, kwa sababu unajua wewe huwezi kufanikiwa kwenye lile eneo ambalo yeye amefanikiwa.

Njia yako ya mafanikio itakuwa tofauti kabisa na ya kwake. Na usisahau kwamba wewe mwenyewe hapo ulipo, pamoja na kuwa na wivu kwa mtu fulani, wapo watu ambao wana wivu na hapo ulipo wewe. Ukifikiria hivi, unaona jinsi ambavyo ni kitu cha ajabu kuwa na wivu kwenye mafanikio ya wengine.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Craving Mind (Jinsi Tunavyonasa Kwenye Uraibu Na Jinsi Ya Kuvunja Tabia Mbaya.)

Tatu; wafurahie wale waliofanikiwa na watumie kama hamasa kwako.

Kama kuna mtu unayemjua na amefanikiwa sana, mtu ambaye hakuna aliyedhani angeweza kufanikiwa kiasi hicho, wala usiwe na wivu, badala yake furahia sana mafanikio yake.

Unapaswa kufurahia mafanikio yake kwa sababu kama yeye ameweza kufanikiwa licha ya ukawaida ambao alikuwa nao, ina maana kwamba kila mtu anaweza kufanikiwa zaidi kama atajua eneo sahihi la mafanikio yake.

Wewe pia unaweza kufanikiwa sana kama utajua eneo sahihi kwako na ukajitoa ili kuweza kufanikiwa zaidi.

Unapokutana na mtu yeyote aliyefanikiwa kuliko wewe, shukuru na furahia sana mafanikio yake. Hiyo itakufanya wewe upate hamasa ya kufanya zaidi. Pia utaweza kujifunza kwake jinsi ambavyo ameweza kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zinawarudisha wengi nyuma.

Uwepo wa watu waliofanikiwa ni hitaji muhimu sana kwa mafanikio ya wengine. Usione wivu, bali furahia na chukua hatua.

Nne; jua eneo ulilo bora, liendeleze na bobea eneo hilo.

Kama tulivyojifunza hapo juu, binadamu wote hatufanani, na alichofanikiwa mwingine, siyo utakachofanikiwa wewe kupitia kitu hicho.

Unachohitaji kufanya ni kuchagua eneo ambalo upo vizuri, ambalo unapenda kufanya na upo tayari kufanya hata kama hakuna anayekulipa.

Ukishajua eneo hili, kazana sana kuwa bora, bobea kabisa kwenye eneo hili. Angalia ni jinsi gani kile unachofanya kinaweza kuwasaidia wengine na wasaidie sana.

Asiwepo mtu mwingine duniani, anayeweza kufanya kile unachofanya kwa namna unavyofanya. Kitu hicho kitakupeleka wewe kwenye mafanikio makubwa pia.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Own The Day, Own Your Life (Imiliki Siku Uyamiliki Maisha Yako).

Tano; kuwa tayari kujifunza kutoka kwa kila mtu.

Utayari wako wa kujifunza kwa kila unayekutana naye utakusaidia sana kuweza kufanikiwa. Hivyo unapokutana na mtu aliyefanikiwa kuliko wewe, pale unapoanza kupata hisia za wivu, jiambie ni kitu gani naweza kujifunza kutoka kwa mtu huyu.

Hata kama kuna vitu vingi haukubaliani naye, wewe angalia kipi unaweza kujifunza. Na kumbuka kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa kila mtu unayekutana naye. Na unapokutana na aliyefanikiwa, ndiyo kazima yapo mengi mno ya kujifunza kwake.

Kuwa tayari kujifunza kwa kila mtu, mwone kila mtu kama mwalimu wako bila ya kujali umri wake au uwezo wake ukilinganisha na wako. Ukiwa mtu wa kujifunza, utaweza kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.

Wivu ni hisia mbaya sana ambayo haina msaada wowote kwako. Usikubali hata kidogo akili yako ikatawaliwa na hisia za wivu, pale unapomwona mtu amefanikiwa sana, furahi na jifunze kupitia yeye. Jua utofauti wako uko wapi na kazana kuwa bora kwenye eneo hilo. Na kumbuka kwamba njia za mafanikio ni nyingi, hivyo unapaswa kuijua njia yako na kuweka juhudi kufanikiwa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha