Leo nakuambia kitu ambacho kinaweza kukuumiza, lakini ukweli lazima usemwe kama ulivyo.

Ni mazoea kwetu kuwa na hofu juu ya fedha, hasa pale ambapo tunakuwa hatuna uhakika na kipato chetu, hatutajijengea uhuru wa kifedha na hatujui kesho itakuwaje.

Labda huna kazi maalumu na hivyo hujui kwa hakika kipato chako cha kesho kitatoka wapi, hilo linakupa kubwa.

Au upo kwenye ajira kabisa, ila kasi ya watu kuondolewa kwenye kazi zao inakupa wasiwasi, unajiuliza vipi kama na wewe utaondolewa, maisha yatakwendaje?

Tatizo kubwa

Au upo kwenye hali ambayo kipato chako hakitoshelezi mahitaji yako, na hivyo kila wakati una hofu maisha yatakwendaje?

Pia inawezekana upo kwenye madeni, na wanaokudai hawana tena imani na wewe, wameshakuchoka na muda wowote wapo tayari kukuchukulia hatua.

Mambo yote hayo yanatengeneza hofu, hofu ambayo inaweza kuwa ngumu kuondokana nayo, kwa sababu ni kitu halisi, ni kitu muhimu, nani asiyefikiria kuhusu fedha?

Lakini ninachokuambia ni kwamba, kuhofu kuhusu fedha ni kupoteza muda wako. Kwa sababu hakuna hofu yoyote ambayo imewahi kumwezesha mtu kuchukua hatua, zaidi ya kumfanya mtu akate tamaa na kushindwa kuchukua hatua.

SOMA; UKURASA WA 869; Kama Haiumizi, Haina Thamani…

Badala ya kuhofia kuhusu fedha, hebu okoa muda na nguvu zako, na zitumie kufikiria ni tatizo gani la watu unaweza kutatua na likakuondoa kwenye changamoto ya kifedha uliyonayo. Angalia thamani ipi unaweza kuongeza kwa wengine kisha fanya hivyo.

Angalia mazingira na watu wanaokuzunguka, kila mtu kuna aina ya msaada anaohitaji kwenye maisha yake, je wewe unaweza kutoa msaada wa aina gani? Toa msaada huo na hilo litakuzalishia fedha.

Ukiacha kuhofu kuhusu fedha na ukaanza kuchukua hatua, siyo tu kwamba matatizo ya fedha yatapungua, bali akili yako itakuwa na utulivu wa kuweza kuona hatua sahihi za kuchukua.

Usiichoshe akili yako kwa vitu ambavyo havina matokeo ya kukuondoa kwenye changamoto uliyopo. Tumia muda na nguvu zako kwa vitu vyenye matokeo mazuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog