The key is to keep company only with people who uplift you, whose presence calls forth your best. – Epictetus
Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri na ya kipekee ya leo.
Ni fursa nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ni mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio mwaka huu 2018.
Asubuhi ya leo tutafakari ZUNGUKWA NA WANAOKUINUA…
Wazazi walipokuwa wanatuambia usicheze na watoto fulani kwa sababu tabia zao ni mbaya, tulifikiri wanatunyima tu kuwa na watu tunaowapenda.
Tulifikiri kwamba tunaweza kucheza nao tu lakini tabia zao zisituathiri.
Lakini ukweli ni kwamba, wale wanaotuzunguka, tabia zao zinatuathiri moja kwa moja.
Hata kwenye utu uzima, unaweza kujiambia kwamba tabia za wale wanaokuzunguka haziwezi kukuathiri, wewe unakaa nao tu lakini huwezi kubeba tabia zao. Lakini ni kujidanganya.
Wale wanaotuzunguka, wale tunaotumia nao muda wetu mwingi, ndiyo wanachangia kuyajenga au kuyabomoa maisha yetu.
Hawa ni watu ambao wana ushawishi mkubwa sana kwetu, ni watu ambao wakirudia kutuambia mara kwa mara kwamba tunachotaka kufanya hakiwezekani, tunajikuta tunakubaliana nao kwamba hakiwezekani.
Kadhalika wakiwa watu wa kutuambia inawezekana, hata kama jambo ni gumu kiasi gani, tunaanza kuona ni kwa njia zipi inawezekana.
Hivyo wajibu wetu namba moja kwenye maisha, ni kuhakikisha tunazungukwa na watu ambao wanatuinua kwenda juu zaidi, na siyo wanaotudidimiza kwenda chini.
Na kigezo rahisi cha kupima mtu kama atakuinua au kukudidimiza ni kuangalia je yupo juu au analwenda juu? Au yupo chini na ameshakata tamaa.
Japo pia kuna ambao unaweza kuona wapo juu lakini wakawa wa kwanza kutaka kukudidimiza, hawa wapo juu kwa mwonekano wa nje tu, ila ndani yao, wako chini na hawajiamini.
Hakikisha unazungukwa na watu ambao tayari wapo juu na wanajiamini, au wanakazana kwenda juu na wanajiamini.
Wale waliokaa chini na kuridhika, watahakikisha na wewe unakaa chini kama wao. Kaa nao mbali sana. Usijidanganye kwamba hawana uwezo wa kukukalisha chini. Wape muda na utashangaa wewe mwenyewe umekaa, usijue ni nguvu gani imekukalisha.
Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha