Every sin is the result of a collaboration. – Lucius Annaeus Seneca.

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ndiyo mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio mwaka huu 2018.

Asubuhi hii tutafakari KILA BAYA NI MATOKEO YA USHIRIKIANO.
Watu wawili wanapogombana au kupishana kauli, ukimsikiliza kila mmoja kwa wakati wake, atakueleza kwamba mwenzake ndiyo kasababisha yote hayo. Yaani ni kama vile yeye hakuna alichochangia, bali mwenzake ndiyo kasababisha na kufanya yote.

Lakini wote tunajua ya kwamba, mtu mwenye akili zake timamu, hawezi kuanzisha ugomvi au ubaya peke yake. Lazima kuwepo na mtu mwingine na lazima mtu huyo mwingine achochee ugomvi huo.
Hivyo lolote baya ni matokeo ya ushirikiano baina ya wale wanaojikuta kwenye baya.

Hata kama unaona umeonewa kiasi gani, jua kwamba na wewe pia umechangia kwenye kuonewa kwako huko.
Unaweza kuona una kila haki ya kumalumu yule anayekufanyia ubaya, lakini ukasahau kuona kwamba na wewe mwenyewe unachangia kwenye ubaya huo.

Hivyo rafiki, unapojikuta kwenye ubaya au tatizo lolote, badala tu ya kulaumu wengine, jiulize wewe mwenyewe umeshirikije kwenye tatizo hilo. Jiulize umechangia na kuchocheaje?
Huenda kuna maneno uliyotoa ambayo yaliamsha hasira kwa wengine,
Huenda umevumilia sana kiasi kwamba watu wamezoea kufanya wanavyotaka.
Pia huenda ni namna unavyochukulia yale wanayofanya wengine.

Unachopaswa kukubali ni kwamba, chochote kinachotokea kwenye maisha yako, kizuri au kibaya, yote umeshiriki kutengeneza.
Hivyo kama unataka kutatua, kama unataka kitu fulani kisitokee sana, jua umeshirikije kisha acha kile ulichofanya ambacho kimechochea hayo yaliyotokea.

Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha