Kuna mtu mmoja amewahi kunukuliwa akisema duniani kuna makundi matatu ya watu, wale ambao wanafanya vitu vitokee, wale ambao wanashangaa vitu vinavyotokea na wale ambao hawajui nini kinachotokea.

Unahitaji kuwa kwenye kundi la kwanza kama unataka kuwa na mafanikio kwenye maisha yako, kuwa kwenye kundi la wanaofanya vitu vitokee, kuwa mtu wa kutengeneza vitu.

Kutengeneza vitu ndiyo njia pekee itakayokusimamisha kwenye dunia hii ya kelele, dunia ambayo kila mtu anaweza kusema, anaweza kukosoa na anaweza kuahidi chochote. Lakini ufanyaji unazidi kuwa mgumu kadiri siku zinavyokwenda.

Kila Mtu

Kuwa mtu wa kutengeneza vitu, mtu wa kuchukua hatua na kuhakikisha maisha yako na ya wengine yanaendelea kuwa bora zaidi.

Sasa ili uweze kutengeneza vitu, lazima uondoke kwenye yale makundi mengine mawili, makundi ya kushangaa vitu vinavyotokea na kutokujua kinachotokea.

SOMA; UKURASA WA 1103; Tatizo Lako Halihitaji Kutumia Chochote…

Kwa kifupi ili uwe mfanyaji, lazima kwanza uache kuwa msemaji pekee. Itapendeza kama utakuwa mtu wa maneno kidogo na vitendo zaidi.

Badala ya kusema mara kwa mara kwamba unataka kuanza biashara, anza biashara, anza kwa hatua ndogo sana kisha endelea kukua kuanzia hapo.

Badala ya kila siku kusema unataka kuandika kitabu, kaa chini na anza kuandika kitabu, weka kwenye maandishi kile unachoona kitawafaa wengine.

Ni kwa kuzalisha vitu ndipo unapata amani ya moyo kwamba kuna kitu umefanya. Ni kwa kuzalisha vitu ndipo wengine wanajua uwepo wako. Ni kwa kuzalisha vitu ndipo unapoacha alama hapa duniani.

Siyo kwa kusema utafanya, siyo kwa kutamani ungefanya, bali kwa kufanya, kwa kuzalisha.

Je wewe ni mzalishaji au msemaji?

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog