“Excellence is an art won by training and habituation. We do not act rightly because we have virtue or excellence, but we rather have those because we have acted rightly. We are what we repeatedly do. Excellence, then, is not an act but a habit.” -Aristotle

Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana kwetu, ni nafasi yetu ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo bora.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa mwaka huu 2018.

Asubuhi ya leo tutafakari UBORA NI TABIA, SIYO TENDO…
Kila mtu anapenda kuwa bora kwenye maisha yake, lakini mchakato wa kufikia huo ubora ndiyo wengi hawauelewi.
Wengi hufikiri ubora ni tukio la mara moja, kwamba unaamka tu na kujikuta umeshakuwa bora.
Au unasoma kitabu na mara moja unakuwa bora.
Au ukipewa ushauri na mtu fulani basi unakuwa bora.

Ubora siyo tendo, bali ubora ni tabia.
Na tabia yoyote ile, inajengwa kwa kujirudia rudia kwa matendo fulani kwa muda mrefu.
Hivyo ili kufikia ubora, lazima uwe mtu wa kuchukua hatua za kuwa bora zaidi mara kwa mara, kila siku na mara nyingi kwa siku.

Kadiri unavyoendelea kuchukua hatua, ndivyo unavyozidi kuwa bora.
Lakini sasa, ubora hauna kilele, huwezi kufika mahali na kusema umeshakuwa bora sana kiasi kwamba huhitaji tena kuwa bora zaidi.
Ukishafika hatua hiyo, jua ndiyo anguko limeanza.

Hata wale ambao kwa nje unaweza kuona ni bora sana, ndani yao wanajua kitu kimoja, kwamba lazima waendelee kuchukua hatua za kuwa bora zaidi kila siku na kila wakati.

Tengeneza tabia ya kuwa bora,
Kila wakati angalia fursa za kuwa bora zaidi na zitumie.
Usisubiri tukio moja la kukufanya kuwa bora,
Fanyia kazi ubora wako kila siku, kwa kuchukua hatua ndogo ndogo kila siku.

Nenda kachukue hatua za kuwa bora zaidi leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha