“A man can do what he ought to do; and when he says he cannot, it is because he will not.” -Johann Gottlieb Fichte
Asubuhi njema mwanamafanikio,
Ni siku nyingine nzuri na bora sana kwetu.
Tumeipata nafasi ya kipekee, ya kwenda kuweka juhudi kubwa, kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA.
Asubuhi ya leo tutafakari HUWEZI KWA SABABU HUTAKI…
Vitu vingi ambavyo unajiambia huwezi kufanya kwenye maisha yako, siyo kweli kwamba huwezi, bali hutaki tu kufanya.
Lakini kwa kuwa utajisikia vibaya kama utakiri hutaki kufanya, basi unajidanganya kwamba huwezi.
Lakini pale hali inapokutaka kweli ufanye, pale ambapo unakuwa huna namna nyingine, chochote ambacho ulikuwa unasema huwezi kufanya, unajikuta unafanya.
Tunao uwezo wa kufanya mengi na makubwa,
Lakini kwa sababu hatutaki kuutumia, huwa tunatafuta kila aina ya sababu ya kuficha uwezo huo.
Asubuhi ya leo fikiri na orodhesha kila ambacho umekuwa unajiambia huwezi, kisha anza kujihoji kwenye kila kitu, je ni kweli kwamba huwezi au hutaki tu kufanya.
Je ni kweli huwezi kuamka asubuhi na mapema kila siku au hutaki?
Je ni kweli huwezi kuanzisha na kukuza biashara yako au hutaki?
Je ni kweli huwezi kuweka akiba ma kuwekeza au hutaki?
Je ni kweli huwezi kupata dakika 10 mpaka 20 za kusoma kitabu kila siku au hutaki tu kusoma?
Wewe jiulize vizuri kwenye kila unachojiambia huwezi kwenye maisha yako, na utashangaa ni kwa namna gani umekuwa unajidanganya maisha yako yoye.
Huwezi kwa sababu hutaki, ukitaka, na mazingira yakitaka kweli, utafanya chochote kinachopaswa kufanywa.
Sasa usisubiri mazingira yakulazimishe, jilazimishe wewe mwenyewe, na hapo ndipo mafanikio yalipo.
Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha