“You may be the only person left who believes in you, but it’s enough. It takes just one star to pierce a universe of darkness. Never give up.” – Richelle E. Goodrich

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari NYOTA MOJA INATOSHA KUIANGAZA DUNIA.
Huwa tunapenda watu watuamini kwenye kile ambacho tunakifanya.
Tunataka watu wengi wakubaliane na sisi ndiyo tuweze kufanya.
Lakini pale tunapokuwa na maono na ndoto kubwa, pale tunapotaka kufanya yale ambayo hayajazoeleka, hatupati watu wa kukubaliana na sisi.
Hapa wengi hukata tamaa na kuacha kufanya, kwa kufikiri hawana watu wa kutosha wa kuwaamini au kukubaliana nao.

Dunia inaangazwa na nyota moja tu ambayo ni jua.
Jua halisubiri mpaka nyota nyingine zote zikubali kuja karibu na dunia na kuangaza, bali lenyewe linaangaza na mwanga wale unatosha kuifanya dunia kuwa na mwangaza.

Hivyo hata wewe unahitaji mtu mmoja tu wa kukuamini, mtu mmoja tu wa kukubaliana na wewe.
Na mtu huyo ni wewe mwenyewe.
Usikate tamaa pale unapokosa watu wa kukuamini na kuamini mawazo yako.
Usikate tamaa pale unapokosa watu wa kukubaliana na wewe.
Kwanza anza kujiamini wewe mwenyewe, amini unaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Pili kubaliana na wewe mwenyewe, usianze kujishuku au kuwa na wasiwasi iwapo utaweza au la.
Kisha chukua hatua, maana imani na kujikubali ulikonako, kunakutosha kabisa kupiga hatua.

Nenda kaiangaze dunia leo kwa nyota yako moja.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha