Nothing is so wretched or foolish as to anticipate misfortunes. What madness is it to be expecting evil before it comes. – Lucius Annaeus Seneca

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ndiyo mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio kwa mwaka huu 2018 ambapo tutaweza kufanya makubwa sana.

Asubuhi ya leo tutafakari UJINGA NI KUTEGEMEA MABAYA YATOKEE…
Kutegemea mambo mabaya yatatokea, iwe ni kwako mwenyewe au kwa wengine, ni ujinga wa hali ya juu.
Hebu tuangalie rafiki, una akili ambayo ina uwezo mkubwa sana, ina uwezo wa kuumba makubwa, ina uwezo wa kutengeneza picha za mambo makubwa na kutengeneza mazingira ya kufikia makubwa hayo kupitia mawazo.
Lakini wewe unachagua kutengeneza mabaya, kufikiria mabaya yatatokea, kuona unashindwa, halafu unapata hicho ulichokuwa unafikiria.

Akili ni yako, na unaweza kufikiri chochote unachotaka, na akili yako ikakuletea kila aina ya rasilimali unayotaka ili kupata unachotaka, lakini wewe unachagua kufikiria kwamba utashindwa, kwamba haitawezekana, kwamba utakosa, na hicho ndiyo unachopata.

Unaanza biashara, una akili ya kuweza kufikiri chochote unachotaka kwenye biashara yako, kutengeneza picha ya mafanikio na kuishi picha hiyo kila siku. Lakini wewe unatengeneza picha ya kushindwa, picha ya hofu na picha inayokukatisha tamaa usichukue hatua kubwa, kwa sababu umeshaona utashindwa.

Rafiki, ni wakati umefika sasa tuache kutumia vibaya akili zetu zenye uwezo mkubwa sana.
Usikubali hata kwa sekunde moja kutegemea mambo mabaya yatokee.

Amua kufanya kitu na kuweka juhudi zako zote, ukitegemea mazuri na makubwa yatatokea, au
Amua usikifanye kabisa.
Lakini kufanya huku unajiambia nafanya tu, lakini najua haitawezekana, ni ujinga na kupoteza muda wako.
Kwa sababu, huwezi kupata matokeo ambayo ni tofauti na fikra zako mwenyewe.

Wanafalsafa walishatuambia tangu enzi na enzi, tunakuwa kile tunachofikiri.
Sasa kwa nini tusifikiri mazuri wakati wote, kwa nini tusifikiri ushindi? Kwa nini tuaifikiri mafanikio? Kwa nini tusifikiri na kutengeneza picha kubwa kwenye mawazo yetu na kuiishi?

Tafakari hili kwa umakini sana asubuhi hii na weka azimio kwamba hutaruhusu tena akili yako yenye uwezo mkubwa, itengeneze kushindwa kwako. Bali utaitumia vyema kutengeneza mafanikio makubwa kwako.

Uwe na siku njema leo, siku ya kutegemea makubwa na kuyapata.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha