Everyone who got where he is has had to begin where he was. —Robert Louis Stevenson
Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Ni matumaini yangu kwamba umeamka vizuri leo, ukiwa na nguvu na hamasa kubwa ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Ni kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUNA MAHALI WALIANZIA…
Kila mtu ambaye amepiga hatua tunayemwangalia, huwa tunafurahia zile hatua ambazo amepiga.
Lakini tunapojiangalia sisi na kuona kwa nini hatujapiga hatua kama zao, huwa tunaona wao ilikuwa rahisi kwao kwa sababu fulani. Au ni nhu,u kwetu kwa sababu fulani.
Ukweli ni kwamba, kila mtu unayemwona amepiga hatua fulani kwenye maisha yake, kuna mahali alianzia.
Kuna sehemu ngumu ambayo alikuwa mwanzoni,
Kuna juhudi kubwa aliweka kuondoka pale,
Na mambo hayakuwa rahisi kwake kama ilivyo rahisi kufikiria kwa nje.
Kila aliyepiga hatua, kuna mahali alianzia, mahali ambapo palikuwa pagumu, palikuwa na changamoto.
Lakini vyote hivyo havikumzuia.
Hivyo hata wewe rafiki, popote unapotaka kufika kwenye maisha yako, kuna mahali utaanzia, na siyo mahali pengine bali hapo ulipo sasa hivi.
Hapo ulipo, ndiyo sehemu sahihi ya kuanzia, ndiyo mahali pazuri pa kuanzia.
Usijiambie kama mambo yangekuwa tofauti au ungekuwa na kitu fulani ndiyo ungeweza kuanza.
Kila ulichonacho hapo ulipo sasa, kinakutosha kuanza.
Na wapo walioanza kwenye mazingira magumu kuliko wewe lakini wameweza kupiga hatua kubwa.
Uwe na siku bora, kama kipo chochote umekuwa unajiambia utakuja kuanza, anza leo, maana unachosubiri hakitatokea.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha