Kuna njia tatu za kuondoka kwenye umasikini,

Njia ya kwanza, mtu ni masikini, anaweka juhudi anapata fedha za kumtoa kwenye umasikini, lakini haichukui muda anarudi tena kwenye umasikini. Na njia hii hutumiwa zaidi na wale ambao wanapata fedha za haraka, ambazo hawajaweka juhudi kubwa, mfano kushinda bahati nasibu au kurithi mali.

Njia ya pili, mtu ni masikini, anaweka juhudi na kupata fedha za kumtoa kwenye masikini, lakini baada ya hapo hakui tena, anafika hatua fulani, kwa nje anaonekana siyo masikini tena, ila kwa ndani hofu ya umasikini ni kubwa kwake, kiasi kwamba hawezi hata kuchukua hatua kubwa, kwa kuogopa kupoteza kile alichopata.

Njia ya tatu, ni mtu kutoka kwenye umasikini na kuendelea kukua zaidi na zaidi na kutorudi tena kwenye umasikini. Hata pale inapotokea amepoteza fedha, bado harudi kwenye umasikini.

Lengo lako isiwe tu kuondoka kwenye umasikini, bali ujue njia zilizopo mbele yako na kujua ipi njia sahihi ya kuchukua.

SOMA; UKURASA WA 434; Chanzo Kikuu Cha Umasikini Au Utajiri.

Usikubali kuchukua njia ya kwanza wala njia ya pili, badala yake njia yako iwe ya tatu. Na utaweza kuitumia njia ya tatu kama utafanya kitu kimoja kila siku, kujifunza na kuchukua hatua mpya kila siku.

Usiridhike haraka kwa hatua yoyote ile ambayo umechukua na ikakupa matokeo mazuri, ukiridhika haraka utaanza kufanya kwa mazoea na kinachotokea ni wewe kupoteza kile ulichopata.

Pia usikubali hofu ikutawale baada ya kupiga hatua ndogo, kwa sababu ukiruhusu hilo hutaweza kuchukua hatua kubwa kwenye maisha yako.

Dunia iko hivi rafiki, kuna kwenda mbele au kurudi nyuma, hakuna kusimama, kama huendi mbele, basi hurudi nyuma. Songa mbele kila wakati, hiyo ndiyo njia kuu ya kuendelea kubaki kwenye mafanikio.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog