“Time is a sort of river of passing events, and strong is its current; no sooner is a thing brought to sight than it is swept by and another takes its place, and this too will be swept away” – Marcus Aurelius
Hongera mwanamafanikio kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni siku mpya na ya kipekee, ambapo tumepata firsa nyingine ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari HILI PIA LITAPITA..
Tunavyojidanganya…
Tukiwa tunapitia hali nzuri na mambo mazuri kwenye maisha yetu, huwa tunataka mambo yaendelee hivyo kwa muda mrefu, na hivyo hatujiandai kwa matokeo tofauti.
Na pale tunapopitia hali mbaya na mambo yakiwa magumu, huwa tunaona kama hatutaweza kuondoka kwenye hali hiyo, kwamba mambo yatazidi kuwa mabaya kadiri siku zinavyokwenda.
Ukweli ni kwamba, hakuna chochote kinachodumu milele, na hakuna hali ambayo itakaa na sisi kwa muda mrefu iwe nzuri au mbaya.
Hivyo tunapokuwa tunapitia hali nzuri, tusijisahaulishe upande wa pili wa mambo, maana hatutadumu kwenye hali hiyo milele.
Na pia tunapopitia hali ngumu tusikate tamaa na kuona hatuwezi kuondoka kwenye hali hiyo, hali hiyo haitadumu milele.
Muda ni kama maji ya mto yanayotiririka, yakishapita yamepita, yanakuja maji mengine.
Matukio tunayokutana nayo kwenye maisha yote yanapita, na yanakuja matukio mengine tofauti kabisa.
Chochote tunachopitia sasa, tujue ni sehemu tu ya mengi, hivyo tusibweteke wala kukata tamaa.
Kila wakati tuwe tayari kwa mabadiliko na mambo mengine mapya kabisa.
Uwe na siku bora sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha