Do external things distract you? Then make time for yourself to learn something worthwhile; stop letting yourself be pulled in all directions.
—Marcus Aurelius.

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari USIKUBALI KUVUTWA KILA UPANDE…
Usipokuwa makini, kwa zama hizi tunazoishi, utajikuta unavutwa kila upande na usiweze kukamilisha chochote.
Kila siku utakutana na kitu kipya,
Utakutana na fursa mpya,
Utakutana na nafasi unayoambiwa ni nzuri zaidi.

Kama hutakaa chini na kukubaliana na nafsi yako ni yapi muhimu kwako, ambayo utayasimamia, utavutwa kila upande na kibaya zaidi ni kwamba mwisho wa siku hutaona umekamilisha nini.

Chukua mfano pale unapoianza siku bila ya kuipangilia, unaiendea siku kwa kufanya kila kinachojitokeza mbele yako.
Utaimaliza siku, ukiwa umechoka sana, lakini hakuna kikubwa ambach9 umekamilisha.

Usikubali kuendesha na mambo ya nje, maana ni mengi na hayaishi, na kila jipya utaliona ni zuri zaidi na linakupita.
Jua ni nini hasa unataka kwenye maisha yako, kijue kitu hicho kwa kina na weka juhudi kubwa ili kuwa bora zaidi.
Halafu acha wengine wasumbuke na mambo yao, usikimbizane na kila kitu.

Siku ya leo iwe bora sana kwako, iwe siku ya utulivu kwako na kuacha kukimbizana na kila kitu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha