Mafanikio yanakuja na hatari moja, kuwa kioo cha wengi, kuonekana na kila mtu na kuhukumiwa na hata wasiokujua vizuri.

Kadiri unavyofanikiwa ndivyo watu wengi zaidi wanajua kuhusu wewe, na ndivyo wengi watakavyohiji, kukupinga na hata kuhukumu chochote unachofanya.

Hali hii imekuwa inapelekea wengi kupenda kujificha, na sehemu nzuri ya kujificha ni katikati ya kundi kubwa la watu.

Ukiwa katikati ya kundi, ukiwa unafanya kile ambacho kila mtu anafanya, hakuna atakayehangaika na wewe, hakuna atakayekazana kukupinga au hata kukuhukumu, huenda wakawepo wachache, ila siyo wengi kama ungekuwa umefanikiwa zaidi.

SOMA; SIKU YA 7; Tiba Rahisi Kwa Walioacha Shule, Walioacha Kazi na Walioacha Maisha.

Kama utajitofautisha na kundi, kama utachagua kuwa bora zaidi, kama utachagua kufanya kitu cha tofauti, kitu cha kipekee, unajiweka kwenye hatari ya kushindwa. Na unaposhinda ndipo kila mtu anauja na maneno tulijua au tulikwambia.

Ogopa sana tabia hii ya kujificha, kabla hujaacha kufanya kitu, jiulize je unaacha kwa sababu huwezi au unaacha kwa sababu hutaki kufanikiwa halafu watu wakuone na kuanza kukufuatilia.

Wewe pekee ndiye unayeamua kama utakwenda juu au utashuka chini. Na wewe pekee ndiye wa kuchukua hatua ya kufanikiwa zaidi. Epuka na acha kujifungia kwa kuogopa kuwa kioo cha wengi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog