“Don’t forget to love yourself.” -Soren Kierkegaard

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari USIAHAU KUJIPENDA…
Ni rahisi sana kuwafikiria wengine kuliko kujifikiria mwenyewe,
Wakati mwingine tunapenda kujitoa kwa ajili ya wengine na kujisahau sisi wenyewe.

Ukweli wa maisha ni kwamba, huwezi kuwafanyia wengine kile ambacho hujifanyii wewe mwenyewe.
Kama unataka kuwapenda wengine, unahitaji kuanza kujipenda wewe mwenyewe kwanza.
Kama unataka wengine wafanikiwe, unahitaji kufanikiwa wewe kwanza.
Na ili kuwaokoa wale waliopo kwenye hali ngumu, inabidi wewe usiwe kwenye hali ambayo wao wapo.

Usisahau kujipenda,
Jali sana afya yako, maana hiyo ndiyo hazina muhimu unayomiliki hapa duniani.
Jali malengo na mipango yako na kila siku ifanyie kazi.
Amini kwenye maoni yako na yasimamie, hata kama wapo wanaokupinga.
Kila siku kazana kuwa bora zaidi ya jana, piga hatua kila siku ili kuwa bora zaidi.
Unaposhindwa, jua siyo mwisho wa safari, bali ni funzo kwenye safari, chukua ulichojifunza kisha songa mbele.

Usisahau kujipenda, maana usipojipenda wewe mwenyewe, hakuna yeyote atakayekupenda.
Uwe na siku bora sana ya leo, siku ya kujipenda na kujijali.

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha