Zipo kauli za kitapeli, kauli ambazo zinatumika kuwahadaa watu, wachukue hatua haraka bila hata ya kufikiri kwa kina.
Moja ya kauli hizo ni hii ya fursa ambayo haitajirudia tena. Watu wakishasikia kauli hiyo wanakimbilia kuchukua hatua, bila hata ya kuchunguza kwa kina.
Kinachotokea baadaye inakuwa hasara kubwa kwao, wanajikuta wameingia kwenye kitu ambacho siyo sahihi, na badala ya kunufaika na fursa, wao ndiyo wanakuwa fursa kwa wengine.

Rafiki, zipo fursa chache sana ambazo haziwezi kujirudia kwenye maisha yako. Na moja ninayoijua, ambayo nina uhakika nayo ni maisha yako. Una maisha hayo uliyonayo tu, muda ulionao sasa ndiyo muda pekee ulionao, hautajirudia tena.
Lakini vitu vingine vyote kwenye maisha, vinajirudia, hata vikikupita, vitakuja tena, au vitakuja ambavyo ni bora zaidi ya hivyo vilivyokupita.
Kama Bilionea Richard Branson alivyowahi kusema, fursa ni kama daladala, ikikupita moja, jua kuna nyingine inakuja.
SOMA; UKURASA WA 978; Mambo Mawili Muhimu Kuhusu Fursa.
Usiyumbishwe na maneno ya kitapeli kwenye fursa, usikimbilie kuingia kwenye fursa ambayo hujaichunguza kwa kina kwa sababu unaogopa kupitwa. Hakuna kinachokupita, ila muda pekee.
Kitu pekee ambacho hupaswi kukipoteza kabisa ni muda wako na maisha yako, na moja ya njia za kuokoa muda na maisha yako ni kutokukimbizana na kila aina ya fursa.
Jua kwa hakika nini unataka kwenye maisha yako, na jua unapataje kile unachotaka kisha jifunze na chukua hatua kufika pale unapotaka kufika. Usiyumbishwe na maneno ya kwamba fursa zinakupita, kama unaweza kutumia vizuri muda wako kwa yale ambayo ni muhimu, hiyo ndiyo fursa yenyewe.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog