Kila biashara huwa inapitia changamoto mbalimbali. Baadhi ya changamoto zinaifanya biashara kuwa imara zaidi kwa sababu mfanyabiashara anajifunza na kuweza kupiga hatua zaidi.
Lakini baadhi ya changamoto huwa zinakuwa kikwazo kikubwa kwenye biashara na kuiweka biashara kwenye hatari ya kufa kabisa. Hizi ndiyo changamoto ambazo wafanyabiashara wengi huwa wanaziogopa kwa sababu hakuna anayependa biashara yake ife.
Zipo njia nyingi za kuiokoa biashara inayotaka kufa kutokana na changamoto mbalimbali. Lakini ipo njia kuu moja ambayo ukiweza kuifanyia kazi vizuri basi biashara yako itaweza kuondoka kwenye changamoto hata kama ni ngumu kiasi gani.

Njia hiyo ni kuuza. Wakati ambao biashara ipo kwenye changamoto kubwa na hatari ya kufa, unapaswa kuweka kipaumbele kikubwa kwenye kuuza. Hii ni kwa sababu kuuza ndiyo njia pekee ambayo biashara inaingiza fedha. Hivyo unapouza ziadi unachangamsha mzunguko wa fedha wa biashara na hilo linatatua matatizo mengi ya kibiashara.
Mzunguko wa fedha kwenye biashara ni sawa na mzunguko wa damu kwenye mwili wa binadamu, na mauzo ndiyo moyo wa biashara. Moyo ukisimama na kuacha kusukuma damu mtu hufa. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye biashara, kama mauzo yatasimama, mzunguko wa fedha unasimama na biashara inakufa.
SOMA; BIASHARA LEO; Watu Hawapendi Kuuziwa, Bali Wanapenda Kununua.
Kosa kubwa wanalofanya wafanyabiashara wengi ni pale biashara inapokuwa kwenye changamoto, wanaacha kuuza, wanaacha kutafuta masoko mapya kwa ajili ya biashara yao. Wanaweza kufanya hivyo wakikazana kupunguza gharama, lakini hilo linachochea biashara kufa zaidi.
Hatua yoyote unayochukua kwenye biashara unayokufa, hakikisha msingi mkuu ni kukazana kuongeza mauzo.
Ndiyo, utahitaji kudhibiti mzunguko wa fedha, ili kuokoa fedha zinazopotea.
Ndiyo, utahitaji kuongeza ufanisi zaidi kwa kila unachofanya kwenye biashara.
Ndiyo, utahitaji kupunguza gharama za kuendesha biashara yako.
Lakini usisahau msingi huu muhimu, hakikisha unauza. Uza. Hili ndiyo muhimu kabisa, ndiyo litakalosaidia mipango mingine uliyoweka iweze kufanikiwa.
Biashara inapokuwa kwenye changamoto, ndiyo wakati mzuri wa kuukazana kuuza zaidi na kuifikisha biashara kwa wateja wapya ambao hawakuwa hata wanaifahamu.
Huu ndiyo wakati wa kufanya zaidi ya ulivyozoea, kwa sababu mazoea hayatakusaidia wakati wa changamoto. Kitakachokutoa kwenye changamoto ni mzunguko wa fedha, ambao unategemea sana mauzo.
Usifanye kosa la kubana matumizi ambayo yatapunguza juhudi za mauzo unazotaka kuweka, punguza kila aina ya gharama unayoweza, lakini usipunguze gharama za masoko na mauzo. Hivi ndiyo njia pekee za kuifanya biashara iendelee kuwa hai.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog