Kwa asili, ukuaji wowote unahitaji muda, tena muda wa kutosha na haraka haijawahi kusaidia.
Tukianza na sisi wenyewe binadamu, mimba inatungwa, inakaa tumboni kwa miezi tisa, baada ya hapo anazaliwa mtoto, ambaye hawezi kujilisha wala hata kusema anataka kujisaidia, inamchukua miaka mitano kuweza kupata ufahamu wa kawaida wa kufanya mambo ya msingi ya maisha yake. Na baada ya hapo, inamchukua miaka mingine 15 mpaka aweze kuwa mtu anayefikiri sawasawa na kufanya maamuzi.

Lakini wewe unataka uanzishe biashara, na baada ya muda mfupi uanze kuvuna faida kubwa kama wale uliowakuta kwenye biashara hiyo. Au umeanza kazi na mara moja unataka vyeo na marupurupu makubwa kwa sababu uliowakuta wanapata hivyo.
Haina tofauti na kuzaa mtoto, halafu siku ya kwanza unashangaa kwa nini hawezi kula mwenyewe na kusema anataka kujisaidia.
Ukuaji wa chochote unahitaji muda, na kadiri kitu kinavyokuwa muhimu na kikubwa, ndivyo ukuaji wake unachukua muda mkubwa.
SOMA; UKURASA WA 627; Haraka Ya Zama Hizi Itakupoteza…
Hivyo usikate tamaa pale unapoweka juhudi lakini huoni matokeo makubwa, kwa sababu juhudi hizo hazipotei, bali zinakuwa msingi wa mafanikio ya baadaye ya kile unachofanya.
Uvumilivu na subira ni vitu muhimu sana, kama unafanya kilicho sahihi na unajitoa kweli katika kukifanya, ukuaji utaendelea kwa asili na baadaye utanufaika na matokeo yake.
Usiwe mtu wa kukata tamaa haraka na kukimbilia mambo mengine yanayoonekana kulipa kwa nje. Chochote unachoona watu wanafanya na kufanikiwa, jua wameweka muda na juhudi, wamekuwa na subira mpaka kufika hapo walipo sasa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog