“We die every day. You see, every day a little bit of our life is taken away from us, and even at the moment we are growing, our life is decaying. We lose our infancy, then childhood, then adolescence.” — Seneca

AMKA Mwanamfanikio,
Amka na ianze siki hii mpya, siku bora na ya kipekee kwako,
Uweze kuitumia siku hii vizuri, uweze kufanya makubwa ili kuweza kupata kile ambacho unataka kwenye maisha yako.

Msingi unaotuongoza kila siku ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA na mwongozo wetu ni TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo hivi viwili vinatuwezesha kuvuka kila aina ya changamoto tunayoweza kukutana nayo.

Asubuhi ya leo tutafakari TUNAKUFA KILA SIKU, KUHOFIA KIFO NI KUACHA KUISHI…
Kila siku tunakufa rafiki,
Na kama anavyotuasa Seneca, kila siku inayopita, kuna kitu tunapoteza kwenye maisha yetu.
Tulianza kwa kupoteza utoto wetu,
Halafu tunapoteza ujana wetu,
Unakuja kupoteza utu uzima wako
Na mwisho kabisa kupoteza maisha yote.
Kila siku kuna kitu cha maisha yetu tunapoteza, na hicho ni kifo kwetu.

Kwa kujua hili, tunapaswa kufurahi na kuwa makini pia.
Tunapaswa kufurahi kwa sababu hatuna haja ya kuhofia kifo kinachokuja kutokea siku moja, lile ni tukio la mwisho tu, mchakato wa kufa unaendelea kila siku.

Tunapaswa kwa makini kwa sababu kila muda ambao tunaupoteza kwenye maisha yetu ni muda ambao tumechagua kufa bila sababu.
Kwa kuwa kila siku tunakufa, basi ni vyema tukafa kwa sababu sahihi, tukafa kwa jambo ambalo lina maana kwetu na wale wanaotuzunguka.

Nikuulize swali, ikiwa utaambiwa una masaa 24 tu ya kuishi, na kwa hakika, baada ya masaa hayo 24 kamili, utakufa kabisa. Je utaanza kutafuta na kufuatilia habari za udaku na mambo yanayoendelea?
Je utatumia nusu saa nzima kuzurura kwenye mitandao ya kijamii ukitaka tu kujua nini kinaendelea?
Je utakaa na kujiambia ‘umeboreka’ na hujui ufanue nini?
Je utaanza kufikiria wengine wanakuchukuliaje au wanafikiria nini kwa unachofanya?
Je utatumia muda huo kuanza kubishana na watu vitu ambavyo hata baada ya mabishano watabaki vile walivyokuwa na wewe utabaki ulivyokuwa?

Naamini mengi katika hayo hutayafikiria kabisa, achilia mbali kuyafanya, pale utakapokuwa unahesabu kila dakika kuelekea kifo.
Lakini cha kushangaza ni kwamba leo utaenda kufanya mengi kati ya hayo, wakati leo pia kuna sehemu ya maisha yako inakufa, sehemu amayo inaondoka na haitarudi tena.

Rafiki yangu, kabla hujafanya chochote na maisha yako na muda wako pia, tafadhali sana jiulize je hichi ni kitu ambacho nipo tayari kiniue? Je ni kitu ambacho nitafanya hata kama zimebaki dakika 30 za mimi kuishi?
Kama jibu ni hapana usifanye, na peleke muda, nguvu na maisha yako kwa yale ambayo ni muhimu zaidi kwako, yale ambayo uko tayari kufa ukiyafanya.

Uwe na siku bora sana ya leo rafiki yangu, siku ya kufanya kile ambacho upo tayari kufa ukifanya.

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha